Nahodha msaidizi wa Azam FC Himid Mao amesema, kikosi kizima kinamorali kubwa ya kupata matokeo mazuri kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) Tanzania Bara dhidi ya Simba mchezo utakaopigwa Jumamosi ya Aprili 29 Uwanja wa Taifa jijini DSM.
Himid amesema, kikosi kipo vizuri na watanufaika na urejeo wa wachezaji muhimu waliokuwa majeruhi.
“Morali iko juu, timu ipo vizuri bahati nzuri wachezaji wenzetu karibia asilimia 90 wapo vizuri na wapo fiti na wako tayari kwa mchezo na naamini kocha atakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua timu yake ya kwenda kucheza mchezo huo,” amesema Himid Mao
Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji na mwenye mashuti makali, aliongeza kuwa mchezo huo utakuwa mgumu licha ya kufanikiwa kuwafunga mara mbili katika mechi mbili zilizopita.
“Usidhani kama mchezo huu wa tatu utakuwa mrahisi kama mara mbili zilizopita tulizoshinda, kwani Simba nayo inajipanga, lakini naamini sisi tutajipanga vizuri zaidi ili kuweza kushinda mechi hiyo inayokuja,” alisisitiza Himid Mao
Himid ambaye amekulia kwenye timu hiyo kwa takribani miaka tisa sasa, alitoa wito kwa mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuwapa sapoti kwani wao ni sehemu muhimu sana katika timu na uwepo wao utawaongezea nguvu zaidi uwanjani ya kuibuka kidedea.
Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo, ambapo tayari kimeshaingia kambini hapo jana.