Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Seif Sharif amekuwa hatoi kauli kali zinazoonyesha uwezo wake wa kukabiliana na misukosuko, lakini hivi karibuni alitoa cheche zake kuonyesha atavuka katika msukosuko unaokikabili chama hicho kwa sasa.
Maalim Seif alishafikia kiwango cha kuwa Waziri Kiongozi, nafasi ambayo ilikuwa ya mtendaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), lakini akavuliwa uanachama na kupoteza madaraka yake yote, akafunguliwa kesi, akawekwa ndani kwa zaidi ya mwaka mmoja, na baadaye kupambana na migogoro ndani ya chama hicho cha upinzani.
Aprili 9 katika mkutano wake na waandishi wa habari, Maalim Seif alionyesha kuwa hata mgogoro uliopo sasa dhidi ya kundi linaloongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba utaisha kwa ushindi.
“Binafsi nimetumia uwezo wangu wote kupigania haki na demokrasia Zanzibar na Tanzania nzima na wananchi ni mashahidi wangu,” alisema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam.
“Nimepatishwa taabu na kufanyiwa uovu mwingi, huku wale walio nyuma ya mipango hiyo wakidhani wataweza kunitisha au kunikatisha tamaa. Wengi walionipangia njama hizo wameondoka na mimi wameniacha niko palepale.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda na kunipa uthabiti wa kukabiliana na yote yanayonikuta.”
Alikuwa ametoa historia fupi ya misukosuko aliyokutana nayo tangu aingie katika siasa.
Maalim Seif, ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hivi sasa anaongoza kundi ambalo linadai linatetea uamuzi wa chama katika mgogoro ambao unazidi kukua kila kukicha.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Profesa Lipumba kutaka kurejea katika nafasi ya uenyekiti, ikiwa ni takriban mwaka mmoja baada ya kujiuzulu nyadhifa zote katika chama.
Aliandika barua ya kujiuzulu Agosti mwaka 2015, lakini mwaka jana alirejea na kuandika barua nyingine ya kufuta uamuzi wa kujiuzulu, jambo ambalo Mkutano Mkuu ulilikataa na badala yake ukaidhinisha uamuzi wake wa kujiuzulu.
Lakini Profesa Lipumba aliendelea kudai kuwa ni mwenyekiti halali, na alizidisha msimamo wake baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuandika msimamo wake kuwa anamtambua mchumi huyo kuwa mwenyekiti wa CUF.
Msimamo huo wa Msajili umezidisha mgogoro na wiki iliyopita wanachama walipigana jijini Dar es Salaam, kiasi cha kujeruhiana.
Kwa mujibu wa kauli ya Maalim Seif, mgogoro huo utaisha kwa upande wake kuibuka na ushindi.
Wakati Maalim Seif akisema hakuna haja ya kukaa na upande wa Profesa Lipumba kumaliza mgogoro huo, wachambuzi waliozungumza na Mwananchi wanasema ni muhimu kwa pande hizo kukutana.
Maoni ya wachambuzi
“Ukiutazama mgogoro huu utaona unatofautiana na migogoro iliyopita,” alisema mwanahistoria maarufu wa Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif.
“Awali, Msajili wa Vyama vya Siasa aliandika barua ya kusitisha ruzuku kwa chama hicho kwa sababu ya mgogoro na kwa sababu suala lenyewe liko mahakamani. Lakini amebadilika tena na kutoa ruzuku kwa upande mmoja. Sasa tumlaumu nani? Inaonyesha kuna upendeleo katika mgogoro huo.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuwaita wahusika na kukaa nao ili kumaliza mgogoro huo.
“Msajili akitumika vizuri anaweza kujua nini hasa kiini cha mgogoro wa chama ili kuepusha watu kuumizana na kufukuzana,” alisema.
Hata hivyo, Profesa wa UDSM, Benson Bana alisema hatima ya mgogoro huo iko kwa wanachama na viongozi, akiwataka viongozi wa makundi hayo watimuliwe.
“Kuna njia nyingi za kuumaliza mgogoro huu, kwanza ni kwa wanachama wa CUF kuwaondoa viongozi wakuu wa kitaifa wanaopingana ambao ni Profesa Lipumba na Maalim Seif,” alisema.
Alisema viongozi hao wakishaondolewa, chama hicho kiweke viongozi wapya kwa sababu waliopo wameshindwa kukaa pamoja na kuumaliza mgogoro huo.
Maalim Seif amepitia katika migogoro mingi, akipambana na chama chake na Serikali.
Maalim Seif alikotokea
Mwaka 1988, Maalim Seif na wenzake sita walifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kutofautiana kimsimamo na chama hicho kabla ya siasa za ushindani kurejeshwa.
Wengine waliofukuzwa pamoja na Maalim Seif ni Machano Khamis Ali, Ali Haji Pandu, Shaaban Khamis Mloo, Khatib Hassan, Soud Yussuf Mgeni, Suleiman Seif Hamad na Hamad Rashid Mohammed.
Baadaye walishtakiwa kwa kosa la uhaini, lakini waliachiwa. Baada ya kuachiwa walianzisha vuguvugu la Kamahuru na baadaye chama cha Zanzibar United Front.
Kati ya mwaka 1989 na 1991, Maalim Seif aliwekwa mahabusu.
Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano iliporejesha siasa za ushindani mwaka 1992, Zanzibar United Front iliungana na Civic Party iliyokuwa ikiongozwa na James Mapalala. Maalim Seif akawa katibu mkuu na Mapalala mwenyekiti.
Lakini chama hicho kikaingia katika mgogoro, Maalim Seif akiongoza kundi lililokuwa linampinga Mapalala, ambaye alimtuhumu katibu wake kuwa alikuwa akitaka kurejesha utawala wa kisultani Zanzibar.
Mzozo huo uliisha kwa Mkutano Mkuu wa CUF uliofanyika mwaka 1994 kumtimua Mapalala.
Baada ya kuondolewa kwa Mapalala, nafasi yake ilishikiliwa na Musobi Mageni hadi mwaka 1999, kabla ya kuchukuliwa na Mwenyekiti wa sasa Profesa Ibrahim Lipumba.
Makada wa CUF waliofurushwa
Mgogoro mwingine ulitokea mwaka 2003 uliomhusisha Naila Majid Jidawi aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini CUF na mbunge wa viti maalum ambaye naye aliukosoa uongozi wa chama .
Mwanamama huyo alifukuzwa uanachama mwaka 2004 na akaamua kwenda mahakamani ambako alishinda na kuendelea na ubunge hadi 2005.
Hapo ndipo ndoto yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kugombea urais Zanzibar ilipoishia na kupotea katika anga za kisiasa.
Fatma Kitwana Mselem (Maghimbi) aliyewahi kuwa mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani 1995-2000, alitofautiana na uongozi na baadaye alikihama chama hicho.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema kuwa Maghimbi alihama baada ya kukosa nafasi ya ubunge kutokana na kuangushwa katika kura za maoni.
“Sisi tunaona hatujapata pengo lolote kwa kuondoka kwao na CUF itaendelea kuwa imara kama awali,” alisema Maalim Seif wakati huo.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, mgogoro mwingine uliibuka. Mbunge wa Wawi wakati huo, Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu walifukuzwa.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mbunge huyo kuwa kwenye msuguano mkubwa na chama. Hamad Rashid alikwenda mahakamani na kufanikiwa kulinda ubunge wake .
Credit - Mwananchi