WAKATI hofu ya kutekwa ikiwa juu, msanii wa Hip Hop Bongo, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ amenusurika kutekwa na watu wasiojulikana, Risasi Jumamosi lina habari kamili. Kwa mujibu wa chanzo makini, Nay alipatwa na maswaibu hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokuwa anatoka kwenye shoo aliyoifanyia Kigamboni jijini Dar.
“Alipiga shoo katika Ukumbi wa G5, akamaliza salama tu, mida kama ya saa 10 alfajiri hivi wakawa wameshamaliza. Wakaanza safari ya kurudi nyumbani kwake Kimara kupitia barabara ya kuzungukia Kibada.
“Kwenye gari Nay alikuwa na jamaa mmoja hivi ambaye ndiye msaidizi wake katika mambo ya mitandao. Nay ndiye aliyekuwa akiendesha mwenyewe.
“Sasa wakiwa hawajafika mbali kutoka ukumbini, walishangaa kuona Noah moja ikionekana kuwafuatilia. Nay alipoona hivyo ikabidi aongeze mwendo,” kilisema chanzo hicho. Kikizidi kumwaga ubuyu huo, chanzo hicho kiliweka wazi kuwa, kuna wakati Nay aliwasha taa kama anataka kukata kushoto, akaona gari ile nayo inawasha taa kama inataka kukata.
Alipoona hivyo, yeye hakukata. Akanyoosha. “Nay alitaka kujiridhisha. Ikabidi aoneshe kama anataka kukata kushoto.
Alipoona ile gari nayo imekata, yeye akanyoosha moja kwa moja kufuata ile barabara ya Kibada. Wakashika barabara kuitafuta ile njia ya Mbagala.
“Wale walipoona gari ya kina Nay haikati imenyoosha, nao wakanyoosha na kuanza kuwafukuzia na hapo ndipo Nay alipojua wale watu waliokuwa kwenye ile Noah hawakuwa wa kawaida, akakanyaga mafuta ya kutosha na bahati nzuri kukatokea gari lingine ambalo liliingia katikati yao, wale jamaa wakapunguza mwendo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Alienda kutoa taarifa Sentro lakini akaambiwa arudi kesho yake (Jumatatu iliyopita) hivyo akarudi zake kupumzika nyumbani.” Baada ya kupata ubuyu huo, Risasi Jumamosi lilizungumza na Nay na kumuuliza kuhusu tukio hilo ambapo alikiri kutokea na kwamba ndiyo anajiandaa kurudi tena polisi kutoa taarifa.
“Ndiyo hivyo bwana mimi kiukweli sasa hivi naishi kwa machale machale hata sielewi wale jamaa walikuwa na lengo gani hasa ila kwa kuwa nakwenda polisi, tuwaachie wao,” alisema Nay.
Hivi karibuni, msanii wa Hip Hop, Ibrahim Mussa ‘R.O.M.A’ na wasanii wenzake watatu walitekwa, wakateswa na watu wasiojulikana walipokuwa Studio za Tongwe Records Masaki jijini Dar.
Baada ya siku tatu, wasanii hao waliachiwa wakiwa katika hali mbaya ambapo jeshi la polisi likaahidi kufuatilia kwa undani sakata hilo ili kuwabaini wahusika.