KATIKA moja ya ngoma zake, mwanamuziki wa Hip Hop Bongo kutoka Kundi la Weusi, John Simon ‘Joh Makini’ aliwahi kudokeza kuwa hivi sinema zetu ni Bongo Movies au Bongo lala? Hapa ndipo hoja yangu ilipo. Nina neno juu ya maandamano ya baadhi ya waigizaji wa sinema za Kibongo jijini Dar kwenye Mitaa ya Kariakoo, katikati ya wiki hii kupinga wizi wa kazi zao na uingizwaji holela wa sinema za nje hasa zile series za Kikorea unaofanywa na maharamia wa kazi za sanaa. Ambazo hutengenezwa kimagumashi na kuuzwa kwa shilingi elfu moja.
Tofauti na sinema zao ambazo huuzwa shilingi elfu nne kwa nakala. Naamini huu ndiyo muda muafaka wa kujadili Bongo Movies maana wameingia wenyewe kwenye kumi na nane. Ieleweke kwamba, sipingi maandamano hayo kwa sababu siku hizi kila anayepinga jambo anaambiwa si mzalendo. Pia sipingi kwamba kuna wizi wa kazi za sanaa. Hapana! Ila nina neno kwao! Inawezekana kabisa wasanii hao wako sahihi lakini haukuwa muda mwafaka au mbinu ya maandamano inaweza isiwe suluhisho sahihi.
Nitaeleza. Mara kadhaa nimekosoa mambo ambayo kama hayatarekebishwa, hata wakiandamana kutoka Dar hadi Kigoma kwa miguu kupinga sinema za kutoka nje ya nchi bado hawatapata suluhu wala Bongo Movies hazitaweza kufunika Prison Break, Empire, Fast And Furious, Into The Badlands, Pirates of Caribbean, Power, The Blacklist, Crisis, 24, 3 Days, Revolution, Arrow, Tyrant, Scandal, Revenge na nyingine nyingi kutoka nje ya nchi. Wakati mwingine tuseme ukweli tu, huwezi kulinganisha sinema au series hizi na Bongo Movies.
Ukifanya hivyo, dunia itakushangaa kwa sababu Bongo Movies zimeshindwa kukidhi viwango kwani hazijafikia hata nusu au robo ya zile za nje! Tukubaliane kuwa kuna mambo yanayohitaji elimu, umakini (seriousness), teknolojia na mengine. Ifahamike pia kwamba kutokana na ukosefu wa mambo hayo, ni kwenye Bongo Movies pekee ambako
jambazi anavua viatu anapovamia nyumbani kwa mtu na lazima avae koti jeusi, refu na miwani nyeusi. Mtu anapigwa risasi mguuni anatoka damu mdomoni. Mtu anatoka kulala huku amepaka make ups. Mlinzi wa geti lazima awe amepoteza f’lani (hamnazo).
Pia ni kwenye Bongo Movies pekee ambako inachukua dakika 20 kwa mtu kuwasha gari na kuondoka nyumbani. Mtu anashuka kwenye gari amevaa shati la njano akifika ndani utamuona ana shati la drafti. Mhusika (mfano Ray) anakumbuka maisha yake ya miaka kumi iliyopita halafu anaonekana mweupe na ameweka nywele waves. Pia mtu anapigwa risasi kwenye part one halafu anakufa part two! Katika hali kama hii, maandamano hayawezi kuleta tija badala yake kuna mambo ya kufanywa kwa umakini ambayo mengi ni ya kitaalam. Ni wakati mwafaka kwa madairekta kuzingatia uhalisia wa mambo na mazingira.
Mazingira katika sinema au series ni ishu kubwa mno kama kweli tunataka kupanua soko letu lifikie duniani kote. Tanzania ni tajiri wa mali asili, lakini mazingira yetu ya asili hayaonekani kwenye sinema zetu. Waigizaji ‘uchwara’ wameng’ang’ania kuonekana mabosi kwenye majumba ya kifahari. Wamesahau kabisa kwamba tuna vijiji, mapori na mbuga zenye mvuto wa aina yake ambazo lazima zitamvutia mtazamaji wa sinema husika.
Basi, hata kama tuking’ang’ania mijini basi vitu kama magari yaonekane ni matoleo ya kisasa na siyo yale ya miaka ya 2,000. Tunajipa aibu isiyokuwa ya lazima. Hivi waigizaji wetu wanajua mtu mweusi ana asili ya mavazi yake hata kama hatuna vazi la taifa? Sasa utofauti uko wapi kati ya sinema ya nje ambayo mhusika anapiga suti na Bongo Movies nako anapiga suti au mwanamke mzuri anavaa kimini hadi inakuwa aibu kutazama sinema na watu wa rika tofauti? Narudia tena, Bongo Movies mmejileta wenyewe kwenye kumi na nane hivyo vumilieni kuchomwa sindano. Kuna tatizo kubwa kwenye eneo la uhalisia wa kiugizaji.
Hapa unakuta msanii anaigiza hadi anaigiza anachoigiza! Ni kama mtu kukimbia spidi hadi unapitiliza nyumbani kwenu au kwako. Tukiacha mambo ya kitaalam ndani ya sinema na hasa matumizi ya vifaa vya kisasa (HD-High Definition), pia kuna maisha binafsi ya baadhi ya wasanii wetu nje ya uigizaji. Huko ndiko kuna balaa kwa sababu msanii anataka kufanya mambo ambayo ni nje ya kamera yaonekane kama ni ndani ya kamera. Wanashindwa kutofautisha. Wanaigiza hadi maisha halisi ya kila siku.
Huko kwenye mitandao ya kijamii ndiyo balaa kubwa kwani hakuna wanachokifanya cha kuwajenga kwenye tasnia hii zaidi ya maonesho ya picha za utupu na mambo ya aibu yasiyo na tija. Mwisho kwa leo, maana nitaendelea kukosoa, wasanii wetu ni lazima wajue, tupo kwenye dunia ya kidijitali. Ukiandamana kupinga sinema za nje kuuzwa kiholela Kariakoo, ujue watu watazifuata kwenye mitandao. Huko ni kuwa na bando lako tu, unajiachia utakavyo. Ubora utakaotokana na mambo niliyoyaeleza, unatosha kulikamata soko la Tanzania, Afrika na dunia bila maandamano au kokoro na mtu. Swali la kutafakari; Je, ni kwa nini enzi za uhai wa Steven Kanumba, Bongo Movies ilikuwa juu? Kwani hakukuwa na sinema na series za nje? Tafakari chukua hatua!