Hatua ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliagi, Profesa Kitila Mkumbo kutwishwa mzigo wa ‘kumtua mama ndoo’, ni sawa na kuvishwa mabomu.
Profesa Mkumbo aliapishwa jana na Rais John Magufuli, na kupewa mzigo mzito wa “kumtua mama ndoo” katika wizara hiyo yenye mzigo mkubwa wa kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa.
Profesa Kitila, ambaye ni mwanachama wa ACT-Wazalendo aliteuliwa juzi kushika nafasi hiyo, ambayo ameikubali licha ya awali kukaririwa akimtaka Rais Magufuli aache kuwateua wasomi katika nafasi za kisiasa ili wafanye kazi zao za utafiti na kuzalisha wasomi wengine.
“Ukipewa kazi na mkuu wa nchi ni kushukuru Mungu na jukumu lako ni kufanya kazi kwa bidii. Na mimi niahidi Mheshimiwa Rais, nitakusaidia wewe na Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha kwamba ajenda yako ya kuwafikia Watanzania na kuboresha maisha tunaifanikisha,” alisema Profesa Kitila mara baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
“Maji ni tatizo namba moja kwa Watanzania. Tafiti zinaonyesha kuwa kweli Watanzania wanataja maji kuwa ni tatizo namba moja. Kwa hiyo tuna jukumu kubwa la kumsaidia Mheshimiwa Rais kadri iwezekanavyo (ili kuhakikisha) Watanzania wengi wanapata maji safi na salama,” alisema.