RAIS John Magufuli ameagiza maeneo yote zilipokuwa nyumba za kota yarudishwe katika miliki ya serikali ili zijengwe nyumba kwa ajili ya makazi ya wananchi. Aidha, amezitaka Halmashauri zilizopanga kuuza maeneo hayo kwa kigezo cha uwekezaji kutafuta maeneo mengine.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika eneo la Magomeni Kota, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 644 za waliokuwa wakazi wa eneo hilo na kusema wakati akiahidi baadhi ya watu walidhani hatatekeleza.
“Niliamua kutoa maagizo kwenye maeneo yote yaliyokuwa yakifanana na Magomeni Kota, Ilala na kwingine yawe chini ya serikali, maana yake yawe chini yangu na pasitokee wa kuyauza. Temeke walianza mchezo wa kutaka kummilikisha mchina kwa kisingizio cha uwekezaji wanaingia uwekezaji, nimesema wakatafute maeneo mengine,” alisema.
Alisema nyumba hizo zitakapokamilika wakazi 644 waliokuwa wakiishi katika eneo hilo kila mmoja atakabidhiwa funguo yake. Alisisitiza kuwa wakazi hao watakukaa bure kwa miaka mitano. “Haiwezekani ndani ya Tanzania inayoheshimu uhuru wa masikini na tajiri ifikie mahali ambapo masikini akikaa mahali pazuri aambiwe aondoke.
Matajiri na masikini wote wanahitaji kuishi mjini,” alisema. Rais alisema hakuna Mtanzania wa daraja la kwanza, la pili au la tatu, ndio sababu majengo hayo yakajengwa katika maeneo hayo na kipaumbele kitakuwa ni watu hao 644.
Akizungumzia maeneo mengine alisema serikali itakayoyachukua itafanya vivyo hivyo, kwani Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume aliweza kujenga nyumba kama hizo katika miaka ya 1970 hivyo haiwezekani wanaojenga sasa washindwe.
Rais Magufuli alisema, Serikali itaanza kujenga nyumba kwa mtindo huo katika maeneo mengine yakiwemo Ilala, Temeke, Iringa, Mwanza, Dodoma na maeneo mengine nchi nzima.
Alisema Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inamuagiza kuimarisha makazi ya wananchi na haikubagua mwananchi wa aina gani na nia yake ni kuleta maendeleo bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
Aliupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kazi unayoifanya nakuongeza kuwa kwa Sh bilioni 20 kujenga majengo hayi ni jambo kubwa. “Ukikuta majengo mengine yanazungumzwa yamejengwa kwa mabilioni mengi ndugu zangu mjue hapo tumeliwa, kwa sababu kama haya majengo ya ghorofa nane, hapo tisa na 12 halafu bilioni 20 zinajenga awamu ya kwanza, mnaweza mkaona ni kwa namna gani ninaposimamia serikali hii kubana matumizi.
Hii ndio maana yake,” alisema. Alisema kama tenda hiyo angekuwa amepewa mtu angeweza kudai bilioni 300. Awali, Waziri Lukuvi alisema tayari ameshaunda timu ya watumishi wa wizara hiyo kutembelea maeneo yote kwa ajili ya kuyaainisha yaweze kutengezewa hati na kukabidhiwa kwa Rais Magufuli kufikia Mei mwishoni.