Ingawa wengi walishangaa Rais John Magufuli alipotengua uteuzi wa Charles Kitwanga, mshangao haukuwa mkubwa.
Sifa ya Kitwanga kwa Magufuli ilikuwa ukaribu wake na kiongozi huyo wa nchi, kama Rais alivyowaeleza wananchi katika moja ya mikutano yake.
Ndani ya chama na Serikali, Kitwanga hakuwa na nguvu ya kuweza kushtua watu kutokana na kuvuliwa uwaziri.
Lakini kwa kijana aliyekulia ndani ya CCM, aliyejitoa kukipagania chama hicho, aliyediriki kuwa mstari wa mbele kushambulia walioonekana maadui wa chama na hata kuwasema hadharani mawaziri walioonekana kuwa mizigo, uamuzi wa kumuengua umeshtua wengi.
Na si kushtua pekee, bali unaonekana kutuma ujumbe kwa mawaziri wengine kuwa lolote laweza kutokea.
Nape Nnauye aliachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Magufuli takribani wiki mbili zilizopita. Alivuliwa wadhifa wake wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyoishikilia kwa takriban mwaka mmoja.
Nafasi hiyo imechukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, nafasi iliyochukuliwa na mwanasheria nguli nchini, Profesa Palamagamba Kabudi.
Hakuna sababu zilizotolewa za kuachwa kwa Nape, lakini aliondolewa asubuhi ya siku ambayo angewasilisha kwa wakuu wake, akiwemo Rais, ripoti ya uvamizi wa kituo cha televisheni cha Clouds Media uliofanywa na kiongozi wa Serikali aliyeambatana na askari waliokuwa na silaha za moto.
Mbali na kuenguliwa, Nape alistahimili kukabiliana na askari kanzu waliotaka kumzuia asizungumze na waandishi wa habari kuhusu kuenguliwa kwake kwa kumtishia bastola, tukio lililomfanya aeleze kwa hisia kali jinsi alivyoisumbukia CCM, na hasa miezi 28 aliyoielezea kuwa ilimlaza “porini” kuikoa CCM iliyokuwa inazama.
Alielezea hayo yote akiwa juu ya gari baada ya Hoteli ya Protea kuzuia mkutano wake na waandishi wa habari.
Akiwa kada aliyejipambanua kama mpambanaji wa ufisadi, miaka kumi iliyopita, Nape alimshambulia kwa maneno makali aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UVCCM, Edward Lowassa kwa madai ya kujihusisha na rushwa katika ujenzi wa jengo la kisasa la umoja huo.
Hata hivyo, Nape alishindwa kuthibitisha madai hayo na hivyo kusimamishwa uanachama wa umoja huo mwaka 2008. Baadaye Rais Jakaya Kikwete alitengua uamuzi huo.
Katika kuendelea kuandamwa na majanga ya kisiasa, mwaka 2010 Nape alipogombea ubunge Jimbo la Ubungo, aliishia katika kura za maoni, badala yake akapitishwa Hawa Ng’umbi ambaye hakummudu John Mnyika wa Chadema.
Kwa mara nyingine, Kikwete alijitokeza kuweka mambo sawa alipomteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi mwaka 2010 na katika Mkutano wa Halmashauri Kuu wa mwaka 2011 akateuliwa kuwa katibu wa itikadi na uenezi.
Akishikilia nafasi hiyo, Nape alifanya kazi na makatibu wakuu wawili ambao ni Wilson Mukama na Abdulrahman Kinana, ambaye walizunguka naye karibu nchi nzima wakishutumu watendaji wa Serikali kuwa hawafuati ilani ya CCM ambayo iligubikwa na kashfa za ufisadi.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kumalizika, Nape aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Sifa hizo zilimfanya Nape awe mmoja wa mawaziri wachache waliokulia ndani ya CCM, lakini waziri pekee aliyepigana kuisafisha CCM katika kipindi ambacho ilikuwa inaonekana kuanza kupotez umaarufu.
Pamoja na kuingia ndani ya Serikali kwa mara ya kwanza, historia ya Nape ndani ya CCM ilimfanya aonekane kuwa na nguvu zaidi ya mawaziri wengine wazoefu katika baraza la sasa kama William Lukuvi (Ardhi na Makazi), Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Dk Mwakyembe (Sheria na Katiba na sasa Habari).
Lakini kuachwa kwake sasa kunaweka maswali kama kuna waziri mwingine anaweza kujisikia salama.
Wasomi watoa mtazamo
Wakizungumzia suala hilo, baadhi ya wasomi walisema kuachwa kwa Nape ni tahadhari kwa mawaziri wengine kuwa makini na Rais iwapo wanataka kuendelea kudumu madarakani.
“Hakuna mtu aliye juu ya chama wala hakuna aliye juu ya Serikali. Hata kama umefanya kazi kiasi gani, ukienda kinyume usishangae litakalokupata,” alisema Salim Hamad ambaye ni mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
“Serikalini kuna kitu kinachoitwa collective responsibility (uwajibikaji wa pamoja), hicho naona kilimpitia pembeni Nape.”.
Hata hivyo, alisema Serikali ya Magufuli haina mwelekeo unaoeleweka kiasi kwamba mawaziri nao wanashindwa cha kufuata.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Profesa George Shumbusho alisema Nape ni kiongozi wa Serikali haiwezekani aipinge hadharani akabaki.
“Haiwezekani kiongozi wa Serikali halafu uipinge hadharani, hiyo ni rahisi tu,” alisema Profesa Shumbusho.
Hata hivyo, Nape hakupinga uamuzi wa Serikali, bali alipingana na uvamizi wa kiongozi wa Serikali kwenye studio za kampuni ya Clouds Media.