AGIZO la Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kujengwa maabara kwa kila shule ya sekondari nchini limebainika kutumika kama mwanya wa watendaji wa serikali kufuja fedha za umma.
Aidha, agizo hilo limebainika kukamilisha miradi mingi ya maendeleo iliyokuwa imepangwa kutekelezwa katika bajeti kwa miaka ya fedha 2013/14 na 2014/15.
Novemba 4, 2012, Kikwete, maarufu JK, aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kujenga maabara kwa kila shule ya sekondari katika kipindi cha miaka miwili kuanzia siku hiyo.
JK alitoa agizo hilo alipohutubia wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi mkoani Singida, waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Itigi.
Alisema maabara za sayansi ni muhimu katika maendeleo ya wanafunzi kujifunza kwa nadharia na vitendo. JK alisema kutokana na umuhimu huo, kulikuwa kunahitajika ushirikiano kama ule ulioonyeshwa wakati wa ujenzi wa shule za sekondari za kata ulioanza mwaka 2006.
Hata hivyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imekosoa utaratibu huo na kufichua ufujaji wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na watendaji wa halmashauri na kukwamisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, wakidai pesa zimeelelekezwa kwenye ujenzi wa maabara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vedasto Ngombale, ndiye aliyefichua kadhia hiyo katika mahojiano na Nipashe kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa.
Alisema kuwa kutokana na tamko hilo la JK, watendaji wa halmashauri walilazimika kuelekeza kwenye ujenzi wa maabara fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo, huku baadhi yao wakipata mwanya wa kufuja fedha za umma kwa kisingizio kwamba wamezielekeza kwenye utekelezaji wa agizo la Rais.
"Kilichotokea lile lilikuwa tamko, lakini katika maeneo mengi hapakuwa na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa jambo hilo," Ngombale alisema.
"Kama unavyofahamu, ili kutekeleza mradi wowote katika serikali, sharti kwamba mradi huo utajwe kwenye bajeti, lakini Mheshimiwa Kikwete, kwa mamlaka aliyokuwa nayo, akatoa tamko la utekelezaji wa jambo hilo.
"Sasa kilichotokea ni kwamba baada ya tamko lile, watendaji wa halmashauri kwa maana ya wakurugenzi watendaji, walichokifanya ni kuchukua pesa kutoka katika kasma mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatengeneza maabara.
"Na matokeo yake, tulipokuja kupitia yale mahesabu baada ya utekelezaji, kukawa kumebainika kuna ufujaji mkubwa wa pesa katika halmashauri nyingi."
Ngombale ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), alisema licha ya tamko hilo kusababisha kutumika kwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo ya maji, mpaka sasa bado kuna halmashauri nyingi hazijakamilisha ujenzi wa maabara, akiitolea mfano halmashauri ya Kilwa anayotoka.
Zipo halmashauri nyingi ambazo bado hazijakamilisha ujenzi wa maabara hali ya kwamba tamko hilo lilitolewa na utekelezaji ulifanyika kwa kuchukua pesa kutoka katika mafungu tofauti tofauti," alisema Ngombale.
Mtoto huyo wa kaka mdogo wa mwanasiasa mkongwe, Kigunge Ngombale Mwiru, alisema agizo hilo la JK lilitolewa bila kuwa na bajeti, hivyo fedha za miradi mingine zilikuwa zinachukuliwa na kuingizwa kwenye ujenzi wa maabara, kinyume cha sheria ya bajeti ya mwaka husika.
"Lakini, katika utekelezaji huo, ndiyo mwanya wa matumizi mabaya ya pesa ulipatikana na sisi tulivyokagua, tumeona ni kiasi gani. Kuna ufisadi mkubwa," alisema.
Credit - Nipashe