MABAO ya mastraika Mbwana Samatta, Saimon Msuva na Mbaraka Yusuf waliyofunga wakati Taifa Stars ikizitambia Botswana na Burundi, imesaidia kuitoa Tanzania shimoni katika orodha ya viwango vya soka vya Shirikisho la Sola la FIFA.
Katika orodha iliyotolewa jana mchana, Tanzania imechupa kwa nafasi 22 kutoka 157 mpaka 135, ikiwa siku chache tangu nyota hao waliotupia kambani kuipa Stars ushindi wa mechi mbili mfululizo wa mechi za kirafiki za kimataifa.
Wakati Tanzania ikipanda kwa nafasi hiyo, majirani wa Kenya wamesogea kwa nafasi 10 juu kutoka ile ya 88 hadi ya 78 kidunia, matokeo ambayo yamechangiwa na ushindi kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na sare dhidi ya Uganda.
Uganda wenyewe wamezidi kuonyesha utemi wao kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kupanda kwa nafasi mbili kutoka ya 74 hadi ya 72 jambo linalowafanya wawe vinara kwa nchi zilipo kwenye ukanda huu.
Kwa mujibu wa viwango hivyo, Misri inaongoza kwa ubora kwa Afrika ikiwa nafasi ya 19 kidunia ambapo inafuatiwa na Senegal iliyopo nafasi ya 30 kwa viwango vya FIFA na Cameroon iliyotwaa ubingwa wa Afrika mwaka huu, ipo nafasi ya 33.
Brazili ndio vinara wa dunia kwa sasa ikiipiku mahasimu wao wa Argentina walishuka nafasi ya pili, huku Ujerumani ikifuatiwa katika nafasi ya tatu.
Nchi za Chile, Colombia, Ufaransa, Ubelgiji, Ureno, Uswisi na Hispania zimekamilisha 10 Bora ya orodha hiyo mpya ya Fifa.