WAKATI Rais John Magufuli akihangaika na mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya nchi, ili kudhibiti uvujaji wa mapato, imebainika migodi imetengeneza hasara ‘feki’ ya Sh trilioni 11 ili kukwepa kodi.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, imebaini kuwa migodi imekuwa ikitengeneza hasara hiyo kupitia mikataba mibovu, ili isitozwe kodi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa wiki hii bungeni, hasara hiyo imekuwa ikitengenezwa kwa kampuni kujirejeshea gharama za manunuzi ya bidhaa za mtaji kutoka katika mapato ya kila mwaka.
“Mikataba mingi ya madini inaruhusu kupunguza gharama za manunuzi ya bidhaa za mtaji kwa asilimia 80 hadi 100 katika mwaka ambao bidhaa imenunuliwa kuanzia hatua za utafiti mpaka uzalishaji. Hatua hii hupelekea kupata hasara mfululizo,” ilieleza taarifa ya CAG.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kati ya mwaka 2011 na 2015 migodi sita iliyokaguliwa ilitoa taarifa ya kupata hasara ya Sh trilioni 10.8 na hivyo kuikosesha Serikali kodi inayokatwa katika faida.
Kampuni iliyotoa taarifa ya kupata hasara kubwa katika miaka hiyo mitano, imeelezwa kuwa ni Bulyanhulu Gold Mines Ltd, ambayo ni Sh trilioni 6.5 na kufuatiwa na kampuni Pangea Minerals Ltd, iliyopata hasara ya Sh trilioni 2.7.
Kampuni ya North Mara Gold Mine yenyewe ilitoa taarifa ya kupata hasara ya Sh bilioni 547.7 na kufuatiwa na Williamson Diamond Ltd iliyopata hasara ya Sh bilioni 538 huku kampuni ya Geita Gold Mine ikieleza kupata hasara ya Sh bilioni 479.
“Serikali inashauriwa kujadiliana na kampuni za madini zinazopata hasara mfululizo ili Serikali iweze kutoza kodi kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mapato ghafi kulingana na sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 2004 (toleo la 2015) na kuhakiki gharama za uwekezaji na marejesho ya kodi, ili kuzuia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi inayotolewa,” alishauri CAG.
Katika mikataba ya uchimbaji madini kati ya Serikali na kampuni za uchimbaji katika migodi mingi ya dhahabu, CAG alibaini kuwa ilisainiwa kabla Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 haijatungwa.
Kutokana na kusainiwa huko, taarifa hiyo ya CAG ilieleza kuwa viwango vya tozo za kodi katika mikataba hiyo vilitokana na sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 na mpaka wakati wa ukaguzi vilikuwa havijabadilishwa kuendana na sheria mpya ya mwaka 2004.
“Kwa mfano, mikataba hiyo inaainisha viwango vya zuio la kodi katika ada ya usimamizi pamoja na huduma za kiufundi kati ya asilimia 3 mpaka 5. Hii ni tofauti na asilimia 15 kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004,” ilielezwa katika taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, CAG aliishauri Serikali kujadiliana na kampuni za uchimbaji madini kupitia kifungu kinachoruhusu kurejewa kwa mkataba kinachopatikana kwenye mikataba takribani yote, ili kurekebisha viwango vya tozo za kodi kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi vinavyobadilika kufuatana na muda tangu kusainiwa kwa mikataba hiyo.