JAJI Lubuva Atoboa Siri za Uchaguzi Mkuu wa 2015 Ulivyokuwa ..Adai Alitishiwa Kifo Amtangaze... ..!!!


MWENYEKITI Mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva amefichua mambo mbalimbali aliyokumbana nayo katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 

Jaji mstaafu  Lubuva, aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2011 na kustaafu Disemba mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage, amebainisha kuwa uchaguzi huo wa mwaka 2015 hatousahau kutokana na kuwapo kwa ushindani mkubwa.

Akizungumza  nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam, alisema mazingira ya ushindani wa kivyama katika uchaguzi huo yalimsababishia hata baadhi ya ndugu zake kumnunia.

Alisema tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992, uchaguzi wa 2015 ulikuwa na ushindani mkubwa kuliko chaguzi zote zilizofanyika nchini.

“Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Agustino Mrema alileta changamoto kama mtu binafsi si chama, mwaka 2015, hali ilikuwa ni nzito kwa kuwa ushindani ulikuwa wa vyama zaidi. Hata hivyo nashukuru Mungu tulimaliza kwa amani, hata watazamaji waliona uchaguzi uliisha kwa amani na baadhi yao nilikuwa nashirikiana nao. Nakumbuka walipokuwa wanaona kampeni walinieleza kuwa ushindani utakuwa mkubwa, najivunia kumaliza uchaguzi ule kwa amani.

“Wakati naingia NEC tulianzisha uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR. Mfumo huo ulikuwa na changamoto zake mojawapo ikiwa ni ucheleweshwaji wa vifaa kwa kuwa vilichukua muda kufika nchini huku Oktoba ilikuwa inakaribia, hata hivyo tulijitahidi kuandikisha kwa kutumia mashine  zilizofika kwa kuhamisha hamisha. Hata wadau wetu walishangaa tumefanikiwa vipi kuandikisha watu milioni 23 kwa muda mfupi ule,” alisema.

 KUNUNIWA NA NDUGU

Alisema kutokana na ushindani huo wa kivyama, baada ya matokeo baadhi ya ndugu zake walimnunia kwa kudhani kuwa haki hakutendeka jambo ambalo halikuwa na ukweli.

“Hata watu wengine ambao ni ndugu zangu walinuna, waliona hawakutendewa haki, lakini ndio kura kwani kwa mujibu wa kura Magufuli ndio kashinda.

“Katika uchaguzi wowote kuna mawili kushinda na kushindwa, anayeshindwa mara nyingi hawezi kuzungumza vizuri juu ya uchaguzi. Ila niseme uchaguzi ule uliendeshwa kwa taratibu na kanuni za uchaguzi, si kweli kwamba kura ziliibwa, kwa sababu tuliendesha uchaguzi kwa uwazi. Kwa mara ya kwanza kura za rais ziliwekwa wazi kwani vituo vyote vilibandika matokeo, hivyo mpiga kura anajua mgombea wake amepata nini ndipo tunaletewa huku Dar es Salaam tunajumlisha na kutangaza.

“Pia mawakala wao wanakuwapo na wanajua mgombea wao amepata kiasi fulani, hivyo niseme kuwa hakuna sehemu jimbo wala wilaya kwamba kura za mgombea urais ambazo zilitangazwa makao makuu hapa Dar es Salaam  ambazo zilikuwa batili. Hivyo unaposema kura zimeibiwa ushahidi upo wapi? Ndio hicho ninachozungumza wakati wote kuwa kadiri matokeo yanapokuja ndivyo nilivyokuwa nayasoma,” alisema.

KUTISHIWA MAISHA

Aidha, Jaji Lubuva alisema licha ya kuwapo baadhi ya kundi la vijana waliomtishia kumuua iwapo kungetokea matokeo wasiyoyataka, anamshukuru Mungu uchaguzi huo ulifanyika kwa amani bila vurugu na kamwe hakuwa na hofu.

“Sikuwa na hofu, tunajua baadhi ya vyama walikuwa na sehemu zao wanaita Ngome, walikuwa wamejiandaa sana kwamba labda kufanya fujo ila nilikuwa nimejiandaa vizuri kwani hata hivi vyama vya upinzani kwa ujumla walishirikiana na chama tawala baada ya matokeo. Kama kweli wangedhamiria kufanya fujo basi wangewachochea vijana wao, na kwa sababu sikufanya lolote baya ndani ya utendaji wangu hapakuwapo na uvunjifu wa amani. Kuna baadhi ya vijana walikuwa wanatishia kuniua iwapo ningetangaza matokeo tofauti na walivyokuwa wakitaka lakini bahati nzuri hapakuwapo na lolote uchaguzi uliisha kwa amani,” alisema.

Licha ya baadhi ya Watanzania kudai kuwa NEC si huru, Jaji Lubuva alisisitiza kuwa Tume hiyo ni huru kwani hata katika kipindi cha uongozi wake hapakuwahi kutokea wito wa Rais kuwataka viongozi hao wafike Ikulu.

 “Nimelizungumza sana tangu nimeingia pale, kwamba yapo madai kwamba Tume si huru, nimesema kwamba hizi ni hisia kwamba Jaji Lubuva ni mteule wa rais na mkurugenzi na makamishna ni wateule wa rais, pia wakati rais huyohuyo ni mwenyekiti wa chama. Lakini siku zote nilisema tume inafanya kazi zake kwa uhuru, hakuna siku yoyote tumeingiliwa na rais na hata sasa nimeicha NEC ikiwa huru. “Kwa sababu tumekuwa tukishirikiana na tume za nchi za EAC na SADC baadhi yao wanajiita tume huru, ila sisi hatukujiita jina hilo ila niwahakikishie kuwa tume yetu ni huru kabisa.

 “Kama mtakumbuka Tume ilikwenda kwa Jaji Warioba kipindi cha kuandaa rasimu ya Katiba, tukawasisitizia kuwa tunafanya kazi kwa uhuru ila kuondoa hayo maono ni vyema kuangalia namna ya kubadilisha kidogo vifungu vya sheria. Kwa sababu pamoja na rais kuteua makamishna, mkurugenzi na hata Jaji mkuu hapakuwapo kabisa na mwingiliano wowote, tangu niwapo pale hata siku moja hatukuwahi kuitwa na rais Ikulu,” alisema

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kwanini hukuweza kuyasema hayo wakatiupo kazini hatutaki ngonjera

    ReplyDelete
  2. Nilifuatilia kwa karibu sana kila ulipotangaza matokeo ya kila jimbo. Mara nyingi hesabu ya kura walizopata wagombea wa kila chama na kura zilizoharibika ilizidi au kutofautiana sana na jumla ya kura zilizopigwa! Simple Math's! Anyways. Yalishapita na MUNGU ambaye ni hakimu wa haki atahukumu kwa haki.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad