Jeshi la Polisi Laongoza kwa Kuwa na Watumishi Hewa..Lawalipa Milioni 757 kwa Mwezi..!!!


JESHI la Polisi nchini limetajwa kuongoza kulipa mishahara watumishi wasiokuwa kwenye utumishi wa umma kati ya taasisi za Serikali katika mwaka wa fedha 2015/16.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matokeo muhimu kwenye ukaguzi wa usimamizi wa rasilimaliwatu na mishahara kwa wizara, sekretarieti za mikoa na balozi kwa mwaka wa fedha 2015/16 umelitaja Jeshi la Polisi kuongoza kati ya taasisi 19 zilizobainika kuwa na tatizo hilo.

Taasisi zinazokaribiana na Polisi zimetajwa na CAG kuwa ni Mahakama na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, huku Bunge likitajwa pia kuhusika.

Katika ukaguzi wake, CAG alibaini kuwa taasisi 19 zililipa Sh bilioni 1.40 za mishahara kwa watumishi 260 walioacha kazi, waliofariki dunia, wastaafu na waliofukuzwa, fedha ambazo zilitakiwa kurejeshwa.

“Jeshi la Polisi limelipa watumishi 139 wasiokuwa kwenye utumishi wa umma likitumia Sh 757,316, 000,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo ya CAG iliyotolewa wiki iliyopita ikifafanua:

“Kati ya fedha hizo, zilizorejeshwa ni Sh milioni 14. 03.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Idara ya  Mahakama inafuatia kwa kulipa watumishi 27 ikitumia Sh 182,913,133 ya tatu ikitajwa kuwa ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji iliyolipa Sh 63,324,829 kwa watumishi 26 na kubainisha kuwa Mahakama tayari imerejesha Sh milioni 35.03 na Wizara ya Maji Sh milioni 47.04.

Ilibainisha kuwa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wasio kwenye utumishi wa umma yalifikia Sh 1,400, 554,592.

CAG alisema mishahara hiyo ililipwa kati ya mwezi mmoja hadi 72 huku taasisi hiyo ya ukaguzi ikieleza malipo hayo kuwa kinyume na kanuni ya 113 ya kanuni za Fedha za Umma za mwaka 2001 (zilizorekebishwa mwaka 2004) inayoagiza maofisa masuuli watunze nyaraka za watumishi ili wanaolipwa wawe ni waliopo na wanafanya kazi.

“Taasisi nyingine ni Bunge ambapo watumishi wawili walilipwa Sh milioni 2.5, Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma watumishi 12,   zaidi ya Sh milioni 150.5, Zimamoto watumishi wanne Sh milioni 2.8 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia watumishi wanane, malipo zaidi ya Sh milioni 62.5.

Pia alitaja Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto watumishi wanane malipo zaidi ya Sh milioni 18.5 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, watumishi wanne Sh milioni 5.3.

Ripoti hiyo ilibainisha taasisi zingine kuwa ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mtumishi mmoja, Sh milioni 22.6 na zilirejeshwa Sh milioni 10, Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera watumishi wanane Sh milioni 12.1 na marejesho ni Sh. milioni 6.7.

Mikoa mingine ni Shinyanga mtumishi mmoja Sh milioni 43, marejesho Sh milioni 22.25, Geita wanne, malipo ni Sh milioni 26.6 na marejesho Sh milioni 17.3, Rukwa watumishi sita, malipo zaidi ya Sh milioni 2.7, Ruvuma wanne Sh milioni 15.8 na Tanga watumishi watatu Sh milioni 3 zilirejeshwa Sh. milioni 1.3.

Ripoti ya CAG ilitaja pia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kulipa mtumishi mmoja Sh milioni 22.4, mkoa wa Manyara malipo Sh. milioni 1.5 kwa mtumishi mmoja huku Mtwara ikilipa mmoja Sh milioni 3.6.

Wabunge

Akitoa maoni kuhusu ripoti ya CAG, Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema pamoja na makusanyo kuwa makubwa kumekuwa na nidhamu ndogo ya matumizi ya fedha.

Kwamba ingawa CAG hajaeleza sababu, lakini hali hiyo inatokana na Serikali kukosa nidhamu katika matumizi.

Alibainisha kuwa kiasi cha fedha kinachotengwa kinakuwa kikubwa lakini matumizi yanapelekwa kwingine akitolea mfano wa ununuzi wa ndege ambao fedha zake hazikuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2016/17.

Alitilia shaka kuwa fedha ambazo zimeainishwa kutumika katika matumizi yanayotiliwa shaka ya kuwepo kwa hali ya rushwa, inawezekana zikawa ndizo zinatumika kuendeshea miradi mikubwa isiyo kwenye bajeti, kwani haijapitishwa kwa utaratibu wa Bunge.

Aidha, alisema kuhusu suala la mashirika ya umma kuna hatari kubwa ya kufilisika kutokana na Serikali kukopa fedha nyingi na kuzipeleka kwenye matumizi yake.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alisema hajamaliza kuipitia ripoti hiyo, hivyo hawezi kuzungumza kwani anahitaji muda wa kuisoma vizuri na kwa umakini akieleza kuwa anatarajia mchango wake kusikika akichangia bungeni.

“Siwezi kuzungumza chochote, bado naendelea kuisoma, mchango wangu nitautoa bungeni,” alisema Bashe.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) alisema ripoti hiyo ni kubwa na imegusa maeneo mengi, akiyataja mikataba ya madini, Tanesco, misamaha ya kodi na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Aidha, alisema hawezi kuzungumza zaidi sasa kwani ripoti ni kubwa na hajui ajikite eneo gani. Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema anahitaji muda kuisoma vizuri.

“Huwa napenda kutoa mchango wangu mapema, lakini kwa sasa CAG amegusa maeneo mengi, hivyo nashindwa nijikite wapi, nahitaji muda kwanza niisome vizuri,” alisema Zitto.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad