NGOJA NIKUONESHE JINSI "MSIBA WA YESU" ULIVYOENDESHWA "KITAJIRI"(YOH. 19:38-42)
1. Watu wawili waliokuwa Matajiri sana ndio waliogharimia Mazishi ya Yesu Kristo. Wa kwanza ni YUSUFU WA ARMATAYA ambae aligharimia KABURI na wa pili ni "Bwana mdogo", NIKODEMO ambae aligharimia MARASHI (Myrrh).
2. YUSUFU WA ARMATAYA anatajwa kwamba alikuwa mtu Msomi wa kiwango cha juu, aliekuwa mashuhuri, mwenye kuheshimika sana na mjumbe wa ngazi ya juu katika Baraza la Utawala la mji (Noble and honourable). Kwa mujibu wa historia ya Wayahudi ni kwamba wajumbe wa mji walikuwa wanapatikana kwa vigezo takribani sita, kigezo kilichotumika kwa Yusufu wa Armataya ni kwa kuwa alitokea katika familia ya kitajiri (Noble Family).
3. NIKODEMO, ambae mimi hupenda kumuita, "Bwana mdogo", ndie yule aliemwendea Yesu usiku kuulizia namna ya kuurithi ufalme wa Mbinguni, kisha Yesu akamwambia auze kila kitu. Japokuwa Nikodemo alikuwa "dissappointed"(alikatishwa tama) lakini tunaona "kumbe" aliendelea kuwa mwanafunzi wa Yesu kimya kimya. Maandiko yanaonesha kwamba Nikodemo nae alikuwa Mjumbe wa Baraza la mji, ingawa cheo chake kilikuwa cha chini ukilinganisha na kile cha Yusufu wa Armataya. Historia ya Wayahudi inaweka wazi kwamba Nikodemo alikua mfanyabiashara mkubwa, tajiri na mashuhuri katika mji ule. Kwa kimombo inaweka vizuri ya kwamba alikuwa, "Young Rich Ruler".
4. Nikikwambia Nikodemo alikuwa tajiri unaweza usinielewe pengine mpaka nikuoneshe thamani ya marashi aliyogharimia kumzikia Yesu Kristo. Tunaambiwa kuwa Nikodemo alitumia marashi (manemane na udi) yenye uzito wa ratli mia moja (100 pounds). Kitu unachotakiwa kufahamu ni kuwa enzi zile, watu mashuhuri na matajiri (wakiwemo wafalme) walikuwa wanazikwa kwa wastani wa juu wa marashi ya ratli 40 pekee. Kwa hiyo, utaona kwamba marashi ya Yesu yaligharimu karibu mara mbili na nusu ya ilivyozoeleka kwa watu maarufu.
Twende kwenye hesabu:
Kwa utafiti niliofanya katika masoko ya marashi duniani ni kwamba, mchanganyiko wa marashi (ya Manemane na Udi), wa uzito wa ratli 100, kwa bei ya sasa unagharimu takribani dola 140,000 hadi 210,000. Hizi ni sawa na takribani shilingi za Kitanzania milioni mia tatu (300,000,000) na kitu hadi milioni mia tano (500,000,000)! Yaani Nikodemo alitoa mchango wa msiba wa milioni mia tano za wakati ule! Usisahau kwamba msiba wenyewe ulikuwa wa ghafla maana hawakutegemea wala kuamini kama Yesu angeuawa, "kiukweli-kwelii". Hebu fikiria vizuri, msiba wa ghafla Nikodemo akamwaga milioni mia tano za wakati ule, je, kungekuwa na kujiandaa? Shikamoo, Nikodemo!
5. Sijajua kama inakuingia akilini kama inavyotakiwa unapoambiwa Yusufu wa Armataya alikuwa mtu tajiri, mashuhuri, mwenye cheo na mwenye kuheshimika. Labda nikuoneshe thamani ya kaburi alilotoa kuuzikia mwili wa Yesu, huenda ukaelewa. Kaburi alimozikwa Yesu tunaambiwa lilikuwa na sifa kubwa tatu (Yoh. 19:41): 1) Eneo la bustani, 2) Limechongwa kwenye mwamba, 3) Jipya kabisa
Makaburi ya hivi walikuwa wanazikiwa Wafalme, Viongozi wakubwa wa Serikali na Matajiri wachache. Rekodi zinathibitisha kwamba makaburi ya staili hii yalikuwa ni gharama kushinda bei ya nyumba na viwanja pale Yerusalem enzi zile. Ukitaka kupata picha halisi angalia bei ya viwanja na nyumba pale Yerusalem hata sasa. (Of course tangu enzi za Ibrahim viwanja vilikuwa ni ghali sana pale Yerusalem)
Bei ya kiwanja cha kawaida cha ukubwa wa mita square (msq) 3,000 pale Jijini Yerusalem, kwa leo, sio chini ya shilingi za Kitanzania Bilioni moja (1,000,000,000). Hivyo, utaona kwamba eneo alilolitoa Yusufu wa Armataya kumzikia Yesu lilikuwa na thamani ya mamilioni ya shilingi kwa wakati ule.
Anyway; Kwa leo sitaki kukupigia hesabu za marashi waliyobeba wale wanawake walioamka asubuhi kwenda kumpaka Yesu kutokana na kuchelewa jana yake wakati kina Nikodemo wakizika. Kumbuka kwamba katika wale wanawake walikuwemo wale ambao ndio walikua wadhamini wakubwa wa huduma ya Yesu (kwa mali zao). Kwa hiyo uwe na uhakika kwamba thamani ya marashi waliyoyabeba nikikupigia hesabu yake utashangaa mwenyewe!
SO WHAT (KWAHIYO NINI SASA)?
1. Ikiwa watu matajiri mithili ya Nikodemo ambao wana jeuri ya kumwaga milioni 500 (za enzi hizo) kwa msiba wa "ghafla" waliamua kumtumikia Yesu; wewe una nini cha maana hata unakuwa na jeuri ya kuubeza Wokovu wa Yesu Kristo? Watu jamii ya Yusufu wa Armataya ambao kugawa nyumba ama viwanja vya mamilioni, tena Jiji la gharama kama Yerusalem, hawaoni shida "still" wanamtumikia Yesu. Wewe ambae nyumba yenyewe unaishi ya kupanga tena na kodi unalipa kwa mbinde; unapata wapi jeuri ya kuukataa wokovu wa Yesu Kristo?
Wewe mwanamke waangalie wanawake wenzako wa kwa Yesu. Walikuwa na mali, walikuwa na fedha (za kwao wenyewe) na wakampokea Yesu na kumtumikia kwa mali zao. Sasa wewe m-dada, m-mama, hela zenyewe huna, maisha yenyewe yanaenda kwa nguvu za kuhongwa, then unabana pua na kuwadharau wanawake wanaomfuata Yesu hapo mtaani kwako na kazini kwako. Whaaaat?!! Hivi unajielewa wewe au ndio unaendaenda kwa dharau zako bila kujua?
2. Ufalme wa Mungu unahitaji watu waliofanikiwa kiuchumi, wenye elimu na wenye ushawishi mkubwa katika jamii kwa sababu hao wanaupa heshima "Ufalme". Kama unamwamini Mungu, mojawapo ya heshima utakayoileta kwenye Ufalme wa Mungu ni kuhakikisha UNAFANIKIWA. Bila kina Nikodemo na Yusufu (wenye hela na vyeo na ushawishi wa kuingia popote), nani angekuwa na uthubutu wa kuuzika mwili wa Yesu? I’m afraid, huenda ule mwili ungeweza hata kuozea msalabani, maana wanafunzi wenyewe walikuwa wameshakimbia na/ama "kujificha".
Sasa wewe Kaka eti unalingia elimu yako ya kuungaunga na kujitia kiburi kutokuupokea wokovu. Elimu yenyewe upo nayo tu wala haijakunufaisha; kibaya zaidi na sasa zilivyosimamishwa ajira upo upo tu halafu unajitia msomi na hautaki kujishughulisha na mambo ya kiroho na kiimani. Watu wenye Mali na wasomi kama akina Yusufu wa Armathaya na Nikodemo walimpokea Yesu, halafu wewe umasikini umekujaa na ujinga na umbumbu kibao unajitia ubishi na kinywinda eti ‘Wanaoenda kanisani hao hao ndio wenye dhambi”. Hivi unajielewa wewe? Unaringia nini wewe?
JITAFAKARI VIZURI
NINAKUTAKIENI PASAKA NJEMA