Jinsi Masaju, Jenista Walivyohangaika na Lissu bungeni


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju jana walikuwa na kazi ya ziada ya kumwongoza Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kuisoma hotuba yake iliyoonekana kuwa na dosari kutokana na kuwa na maneno yenye ukakasi. 

Hali hiyo iliibuka baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kumwita Lissu kuwasilisha hotuba yake. Kabla ya kuanza kusoma, Jenista ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Serikali alimuomba Mwenyekiti kuizuia hotuba hiyo kwa kuwa imejaa maneno ambayo masuala yake yapo mahakamani na pia amezungumzia mwenendo wa Rais, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni za Bunge. 

Alisema hotuba hiyo ina mambo mengi yanayokiuka kanuni. Alisema katika hotuba hiyo kuna mambo ya mienendo ya kesi ambazo zipo mahakamani, jambo ambalo ni kinyume na kanuni na pia, kuna mambo yanayozungumzia mwenendo wa Rais, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni Kifungu 64 (1) (e). “Naomba nitoe utaratibu ni kwanini hoja hii irudishwe mezani kwako na maeneo yanayokiuka kanuni hizi yaweze kuondolewa na ndipo iweze kuwasilishwa ndani ya Bunge hili,” alisema Waziri Mhagama. 

Hata hivyo, Chenge alimruhusu Lissu kusoma hotuba yake huku akimtaka Waziri Mhagama kuainisha maeneo yaliyokuwa na maneno yenye ukakasi. Wakati huo Lissu alianza kusoma hotuba yake, lakini Chenge alimkatisha na kumtaka kuyafuta maneno hayo, kwa kuwa hayapo kwenye hotuba yake na kumtaka kwenda moja kwa moja kwenye hotuba. 

Akisoma hotuba hiyo, Lissu alisema hiyo ni mara yake ya saba kusimama mbele ya Bunge kutoa maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria na ameshangaa kuona Wizara hiyo imekuwa ikiongoza kwa kuwa na mabadiliko mengi ya mawaziri kuliko wizara nyingine. Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, alianza Celina Kombani (sasa marehemu) kisha wakafuata Mathias Chakawe, Dk Asha-Rose Migiro, Dk Harrison Mwanyembe na sasa Profesa Palamagamba Kabudi. 

Alisema ingawa Profesa Kabudi anaweza kuwa mgeni bungeni, lakini si katika uelewa wa matatizo makubwa ya kisiasa na kikatiba nchini. Alimkumbusha majukumu makubwa na mazito anayolazimika kuyabeba kwa nafasi yake hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad