Dar es Salaam. Wakati Taifa likiwa katika simanzi na taharuki baada ya askari wanane kupoteza maisha katika shambulizi lisilo la kawaida dhidi ya Jeshi la Polisi, mashuhuda wa tukio hilo wanasema wauaji walijipanga katika maeneo matatu tofauti katika eneo la tukio kabla ya kufanya shambulizi hilo.
Habari za shambulio hilo la aina yake lililotokea juzi ziliripotiwa na gazeti hili pekee jana na hali ya simanzi ilitawala jana wakati Jeshi la Polisi likitoa taarifa kuhusu tukio hilo, huku Rais John Magufuli akiongoza waombolezaji.
“Baada ya kusikia hili tukio nilikaa kama dakika kumi natafakari bila kupata majibu. Hivi haya matukio yanafanywa na kina nani? Wanafanya kwa malengo gani?” alihoji Othman Juma, aliyekuwa anafuatilia mkutano huo wa Jeshi la Polisi katika ukurasa wa Mwananchi.
Wauaji hao walimshambulia kwa risasi tano dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser (pickup) na wakati askari walipokuwa wanajariku kuruka kujinusuru, watu hao waliwatungua kwa risasi wakati gari likienda kunasa pembeni ya barabara.
Watu hao walilifuata gari hilo liliposimama na kuwavua fulana za kuzuia risasi kisha kuwamalizia tena kwa risasi kabla ya kuchukua silaha saba walizokuta, tatu zikiwa za masafa marefu.
Waandishi wetu waliofika eneo la tukio wamesema hofu imezidi kutanda kwenye vijiji vya Wilaya ya Kibiti, na hasa Kijiji cha Jaribu ambako viongozi wao hawaonekani na wakazi hupotea inapofika nyakati za usiku kuhofia maisha yao.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliiambia Mwananchi kuwa washambuliaji hao walikuwa watatu na walijificha katika maeneo matatu kando ya Barabara ya Dar-Kibiti kuhakikisha hawawezi kulikosa kwa risasi gari hilo la Jeshi la Polisi.
Alisema wakati gari hilo likipita kwa mwendo wa kasi majira ya saa 12 jioni eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa, likiwa limetokea Jaribu Mpakani, kijiji kilichopo takriban kilomita tatu kutoka eneo la tukio, washambuliaji hao walianza kufyatua risasi mfululizo, hasa kumlenga dereva.
“Wauaji hao walifanya mashambulizi hayo wakitokea vichakani kwa kuwa eneo hilo ni pori. Lakini eneo walipouawa askari hao lilikuwa limefyekwa vizuri kwa miti yote na majani kukatwa,” alisema.
Alisema baada ya dereva kushambuliwa, gari lilianza kuyumba na kupoteza mwelekeo na askari waliokuwa ndani walianza kuruka nje ya gari ili kujiokoa au kurudisha mashambulizi na kila waliporuka walikumbana na risasi.
Shuhuda huyo alieleza kuwa baada ya gari kusimama, watu hao walienda kwenye gari hilo lililokuwa limeegemea kwenye ukingo ulio kando ya barabara na kuwamalizia kwa risasi askari hao wanane na mmoja alijeruhiwa mkono wake wa kushoto.
Askari huyo alimudu kuwatoroka wavamizi hao baada ya kutambaa kupanda gema lililokuwa karibu na eneo ambalo gari liligota na kuibukia upande wa pili ambao una mtaro.
“Sielewi. Ni Mungu tu,” alisema askari huyo aliyetambulishwa kwa jina la PC Fredrick ambaye amejeruhiwa mkono wa kushoto.
Lakini dereva wa gari hilo, ambaye pia alijaribu kutoroka eneo hilo, alionekana kirahisi na washambuliaji kwa kuwa alikimbia kunyoosha njia kulingana na mwelekeo wa barabara hiyo na hivyo kushambuliwa kwa risasi nyingine.
Waandishi wetu waliofika eneo la tukio kuanzia jana asubuhi wameeleza kuwa wananchi walisikia milio ya silaha nzito majira ya saa 12:15 jioni, lakini walishindwa kusogelea kutokana na vitendo vya mauaji vinavyoendelea maeneo yao.
Wakazi wa eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa walisema walisikia milio ya silaha nzito tofauti na milio ya bunduki za kawaida na hivyo kuamua kutotoka nje.
Mkazi wa Mkengeni, Rashid Mohamed alisema hofu imezidi kijijini hapo na wanashindwa kufanya biashara zao kama walivyokuwa wakifanya awali, na hivyo maisha yanazidi kuwa magumu.
Mohamed alisema juzi walisikia milio ya bunduki na risasi moja iliangukia kwenye paa la duka lake. Alisema ana hofu kwa sababu biashara yake haiendi vizuri kwa kuwa watu hawaendi kazini kwa kuhofia usalama wao.
“Leo watu wengi hawajaenda kabisa mashambani. Kila mtu ana hofu. Unaweza kwenda halafu ukakutana na hao wauaji. Hali si nzuri kabisa, sijui hatima yangu ni nini,” alisema mfanyabiashara huyo.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Bungu, ambako kuna kambi maalumu ya polisi, Mwajuma Said alisema kwa sasa hawana viongozi kwa kuwa wote wamekimbia baada ya kutishiwa maisha.
Alisema kutokana na kukosa serikali tangu Februari mwaka huu, walianza kupeleka matatizo yao Kituo cha Polisi cha Bungu. Alisema baada ya tukio la juzi hawajui watapeleka wapi shida zao kwa sababu polisi ambao wanawategemea nao wanauawa.
“Walikuja wakatupa vipeperushi kwenye ofisi ambavyo waliandika kwamba wamefika kijiji chetu kwa ajili ya kumuua mwenyekiti, mjumbe na mtendaji wa kijiji. Baada ya vitisho hivyo, viongozi hao walikimbia kijiji hiki, mpaka sasa hatuna serikali,” alisema mwanamke huyo.
Mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wauaji hao wamekuwa wakielekeza mashambulizi yao kwa watumishi wa umma, jambo ambalo linampa hofu.
“Hatujui hatima yetu itakuwaje. Baadhi ya walimu wanaomba uhamisho ili waondoke eneo hili. Polisi tunao wa kutosha lakini yanapotokea mauaji kama haya tunashindwa kujua ni nguvu gani waliyonayo wauaji hao,” alisema mwalimu huyo mkazi wa Kijiji cha Bungu.
Hali ilivyokuwa jana
Mwananchi ilikuta polisi wakiwa eneo la tukio majira ya saa 4:30 asubuhi, wakichukua vipimo, huku baadhi yao wakiwa wameficha sura kwa kuvaa kinyago kinachoruhusu macho pekee kuonekana.
Eneo hilo ni kilomita tatu kutoka kituo cha ulinzi ambako askari hao walibadilishana lindo na kuanza safari ya kurudi kambini Bungu.
Eneo la tukio hilo ni mteremko uliopo Kijiji cha Mkengeni kilichopo kati ya Mkuranga na Rufiji.
Askari mmoja wa kambi maalumu iliyopo Bungu aliiambia Mwananchi kuwa risasi tano zilipigwa mfululizo upande wa dereva kabla gari hilo halijaacha njia na kwenda kuegemea kwenye ukingo wa bonde dogo lililo pembeni ya barabara.
“Sehemu lilipotokea tukio ni kama ina kichaka na askari aliyenusurika alitambaa kwa tumbo kwenye kichaka cha upande wa kulia kama unaelekea Rufiji na kufanikiwa kujinusuru, ingawa alikuwa ameshapigwa risasi ya mkono,” alisema askari huyo.
Alieleza zaidi kuwa baada ya gari kupinduka na askari hao kupigwa risasi, bado walivuliwa vikinga risasi na kupigwa risasi nyingine.
Akizungumza eneo la tukio Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimwambia Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba kuwa washambuliaji hao walijipanga maeneo matatu na walikuwa wanafahamu wanachofanya.
“Wangemkosa hapa, wangempata pale au pale. Lengo lao ilikuwa kumshambulia dereva,” alisema Ndikilo huku akionyesha kwa mikono aliposimama mshambuliaji mmoja baada ya mwingine.
Wananchi katika kijiji cha Mkengeni walikuwa wamesimama katika makundi na wengine wakiwa kwenye vibanda vya kahawa wakijadiliana kuhusu tukio hilo na wengi hawakutaka kuongea na waandishi wakionekana kuhofia maisha yao.
Baada ya Waziri Mwigulu kuwasili eneo la tukio na kupokea maelezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, msafara huo ulielekea Kijiji cha Bungu kuona kambi hiyo maalumu.
Kambi hiyo imetengenezwa kwa maturubai sita ambayo wanaishi askari hao.
Shambulio hilo ni mwendelezo wa matukio kadhaa dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi ambayo yamekuwa yakitokea tangu mwaka juzi. Januari 20, 2015, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri wilayani Rufiji na kuua askari wawili waliokuwepo kituoni hapo na kuondoka na silaha walizokuta.
Uvamizi kama huo ulifanyika Februari 3, 2015 wakati kundi la watu wasiojulikana lilipovamia Kituo cha Polisi cha Mgeta wilayani Kilombero na kuchukua bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi 30.
Tukio jingine lilitokea Julai mwaka juzi wakati watu wasiojulikana walipovamia Kituo cha Polisi Sitakishari, Ukonga, Dar es Salaam na kuua askari wanne na raia watatu na baadaye kupora silaha ambazo idadi yake haikuwekwa bayana.
Katika shambulizi jingine lililofanyika Agosti mwaka jana, polisi wanne waliuawa wakiwa Benki ya CRDB, Mbagala, Dar es Salaam ambako walikuwa wakibadilishana lindo. Watu wasiojulikana waliowasili eneo hilo kwa pikipiki tatu, waliwafyatulia risasi askari hao na kuwaua baadaye kuondoka na bunduki mbili.
Polisi pia wameuawa katika matukio ambayo walijaribu kupambana na watu hao, likiwamo la Vikindu ambako ofisa wa polisi wa cheo cha ASP, Thomas Njuki alipigwa risasi wakati polisi ilipoenda kukamata watuhumiwa wa ujambazi.
“Tumeshapoteza askari zaidi ya 10. Ninaamini wanatosha. Sasa tunaenda kwenye operesheni maalumu, hatutakuwa na mzaha wala msamaha,” alisema kamishna wa operesheni na mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani alipoongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
“Tutawapata popote walipo, tutawashughulikia kikamilifu hakuna atakayebaki. Mapambano haya hayana mwisho, huu ni mwanzo usio na mwisho,”alisema.
Alisema baada ya mauaji hayo ya polisi, operesheni kali ilifanikisha kubaini maficho ya muda ya watu hao.
Kamishna Marijani aliwataja askari waliouwawa katika shambulio hilo kuwa ni Peter Kigugu, ambaye ni mkaguzi msaidizi wa polisi, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zacharia, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub.
Alisema katika msako huo, polisi waliwaua watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kukamata bunduki nne, mbili zikiwa zile zilizoporwa kwa askari.
Alisema watu hao walifanikiwa kuua askari wengi kwa sababu walikuwa pamoja ndani ya gari, na si kwa sababu wana ujuzi wa kipekee.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wa shambulio hilo na ugaidi, Kamishna Marijani alisema: “Wale ni majambazi, hawana lolote. Si chochote. Hatuwezi kuweka kanda maalum kwa sababu yao. Wameamua kupambana na Jeshi la Polisi kwa sababu tunawazuia. Huu si ugaidi, ni ujambazi.”
Alisema matukio ya uhalifu yametawala mkoani Pwani kutokana na kuwa na mapori yanayowavutia wahalifu na kuweka maficho yao.
Kamishna Marijani aliwataka wananchi kuliunga mkono Jeshi la Polisi katika operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa.
Kamishna pia alipiga marufuku pikipiki kuonekana Kibiti, Mkuranga na Rufiji kuanzia saa 12:00 jioni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema watu hao waliiba silaha saba, nne zikiwa ni bunduki aina ya SMG na bunduki tatu za masafa marefu.
Alisema bunduki nyingine mbili aina ya SMG zilizokuwa sehemu ya mbele ya gari la polisi zilipatikana kwa kuwa washambuliaji hao hawakuziona.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alitembelea eneo hilo na kusema wanaofanya mauaji hayo watashughulikiwa.
“Hatukubaliani na jambo hilo, halina nafasi. Mkuu wa Mkoa pokeeni pole na fungeni mikanda upya ili tuunganishe nguvu kukabiliana na uhalifu huu,” alisema Mwigulu akiwa katika kambi maalumu ya Bungu muda mfupi baada ya kuwasili eneo la tukio saa 7:00 mchana.
Waziri Mwigulu aliwapa pole polisi na kuwataka kusonga mbele ili kuhakikisha silaha zilizoibwa zinarudishwa.
Akizungumzia zaidi tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo alisema ni tukio zito kwa mkoa kupoteza askari wanane wakati mmoja. “Ni tukio zito na mtihani mkubwa kwa wananchi, hasa wanapoona askari walioletwa kuwalinda nao wamefariki,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wananchi wawe na subira wakati serikali ya mkoa ikiendelea kulifanyia kazi suala hilo.