Kauli ya Rais Magufuli kuhusu kuuwawa kwa askari Kibiti Rufiji


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi 8 waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni tarehe 13 Aprili, 2017 katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.

Askari Polisi hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria na wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi.

Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.

“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu 8 ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu. “Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amelaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo.

Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ni vizuri Raisi wangu. Ningekushauri ufanye hivyo pia unaposikia Watanzania na raia wakawaida wanapotekwa, kuuwawa, kama maiti zilivyokutwa mtoni bila kubagua na kuingiza siasa. Uchungu ni uleule, Unaposimama kukemea Watanzania wanaona umeguswa. Lakini unachagua matabaka ya watu. Mesegi mbili tofauti. Mauti ni mauti. Ujambazi ni ujambazi. Utekwaji unaua pia. Ahsante.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad