Baada ya kubadilisha katiba, CCM inaonekana kuendelea kujipanga kukabiliana na ongezeko la upinzani nchini baada ya kuteua makatibu wa mikoa na wilaya, wanaoelezewa kuwa “majemedari” waliopewa jukumu la kukipitisha chama katika mtihani wa kwanza wa uchaguzi wa ndani.
CCM inatarajia kuanza chaguzi za ngazi za chini za ndani wakati wowote kuanzia sasa na kukamilisha baadaye mwka huu itakapochagua wajumbe wa vyombo vya juu vya maamuzi.
Mtihani wa pili utakuwa uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa mwaka 2019 kabla ya kumalizia na Uchaguzi Mkuu 2020.
Ikiwa imetingishwa na Uchaguzi Mkuu uliopita, tayari CCM imeshapunguza idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24, na wa Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi 160.
Imeondoa nafasi zisizo za kikatiba katika wilaya na jumuiya zake na kufanya mabadiliko ya sekretarieti. Na sasa imetangaza makatibu wa mikoa na wilaya.
“Hao ndio majemedari waliopewa jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mafanikio,” alisema kada mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, CCM ilipoteza mawaziri wakuu wawili wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye ambao walifuatwa na makada wengine kadhaa wakiwemo wenyeviti wa mikoa, wilaya, wabunge na madiwani.
Pia CCM iliruhusu vyama vya upinzani, hasa vilivyokuwa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupata zaidi ya viti 100 vya ubunge, viti zaidi vya udiwani na halmashauri 19.
Baadhi ya watendaji wa chama hicho hasa makatibu wa mkoa na wilaya, ndio wanaodaiwa kusababisha CCM kupata ushindi mdogo katika Uchaguzi Mkuu uliopita ambao ulikuwa na msisimko mkubwa.
Mwenyekiti John Magufuli alisema waziwazi kuwa makatibu hawakusaidia wakati wajumbe wa Halmashauri Kuu walipoimba wimbo wa kuwa na imani na Lowassa baada ya jina lake kukatwa na Kamati Kuu.
Hivyo, haikuwa ajabu kwa CCM kupanga upya safu ya uongozi kuondokana na masalia ya wasaliti, hasa wanaomuunga mkono Lowassa na wenzake.
Mapema wiki hii, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitangaza majina mapya ya makatibu wa mikoa na wilaya. Kati yao wamo 31 wa mikoa na 155 wa wilaya. Hata hivyo majina yaliyotangazwa ni ya upande wa Bara pekee.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Polepole alisema uteuzi uliofanywa umezingatia weledi, jinsia na mpango wa kuachiana vijiti kwa kuzingatia rika.
Alisema kati ya makatibu hao walioteuliwa wa mikoa. kumi na moja ni wale waliopandishwa hadhi kutokana na utendaji wao, na 20 ni wapya kabisa.
Uteuzi huo umefanyika baada ya chama hicho kupitia ripoti ya tathmini ya uchaguzi uliopita na kubaini baadhi yao walikisaliti chama wakati wa Uchaguzi Mkuu na kusababisha kupoteza viti vingi vya ubunge, udiwani na baadhi ya halmashauri.
Uteuzi huo ni mwendelezo wa CCM kuweka majemedari wapya. Mwenyekiti alianza kupanga safu ya uongozi kwa kuwaondoa Rajab Luhwavi, aliyekuwa naibu katibu mkuu bara na nafasi yake kuchukuliwa na Rodrick Mpogolo, na Nape Nnauye, aliyekuwa katibu wa itikadi na Christopher Ole Sendeka akapewa usemaji wa chama.
Wengine walioondolewa ni Pindi Chana, aliyekuwa katibu wa NEC wa siasa na uhusiano wa kimataifa na nafasi yake kuchukuliwa na Kanali Ngemela Lubinga. Pia Vuai Ali Vuai, aliyekuwa naibu katibu mkuu Zanzibar, Dk Muhammad Seif Khatib na Zakhia Meghji. Nafasi ya kiutendaji ambayo haijaguswa ni ya katibu mkuu.
Makatibu hao kwa mujibu wa katiba ya CCM wana jukumu la kujua takwimu zote za chama katika maeneo yao ya kazi, ikiwamo idadi ya wanachama, matawi, mali za chama, kuandaa uchaguzi wa ndani na kufanya tathmini ya mgombea anayekubalika kwenye eneo lake.
Vigogo 12 wa chama hicho walifukuzwa uanachama kwa usaliti, akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba na wenyeviti wanne wa mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Shinyanga na Mara.