Kwa taarifa za uhakika kutoka Dodoma, kupitia kikao cha Kamati ya Kanuni ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki utafanyika kama ilivyotangazwa na Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai kwa kuzingatia Ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kikao chake kilichoketi jana hadi majira ya saa nne usiku, taarifa hizo zinathibitisha kuwa ombi la KIONGOZI MKUU wa ACT, kutaka chama hicho kipewe haki na nafasi ya kuweka mgombea uchaguzi wa EALA, limetupiliwa mbali kwa sababu halikuwa na mashiko ya kimantiki wala msingi wa kikanuni.
Kiuhalisia kamati hiyo imeungana na Spika Ndugai na kumpongeza kwa kusimamia kanuni za uchaguzi huo hasa kwa kuzingatia msingi wa Kanuni ya 12 inayosema kuwa Uchaguzi wa EALA utafanyika kwa kuzingatia uwiano wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Chama kama ACT chenye mbunge mmoja katika Bunge la lenye idadi ya wabunge 393 ni sawa na 0.00% ambayo ni sawasawa na kiti au viti 0. Kwa hiyo taratibu zinakiengua kuwa katika mchakato wa kugombea hata nafasi moja.
Vile vile kanuni ya 5(5) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge inasema "chama chochote cha siasa chenye HAKI ya kusimamisha mgombea wa EALA kinaweza kuweka wagombea watatu katika makundi ya wagombea ubunge."
Mantiki ya hoja kutokana na msingi huo wa kikanuni, inaonesha kuwa vyama vingine tofauti na CHADEMA, CUF na CCM, haviwezi kusimamisha wagombea kwa sababu havikidhi kigezo cha Kanuni ya 12 ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimsingi Spika amesimamia haki iliyokuwa inaporwa au kupokwa katika chaguzi za EALA zilizopita. Kwa uamuzi huo bila shaka sasa uchaguzi utahusisha vyama vitatu ambavyo ni CCM (6), CHADEMA (2) na CUF (1) ambavyo ndivyo vinakidhi vigezo vya kuweka wagombea.
Ibara ya 50 ya Mkataba wa wa EAC, inaelekeza na kutoa mamlaka kwa kila bunge la nchi mshirika kuchagua wawakilishi kwa mujibu wa kanuni za bunge la nchi husika na huo ndio utaratibu uliopo sasa ambao wapeleka maombi wanaujua vyema.
Ni wazi pia uamuzi huo utakuwa umezingatia masuala mengine ambayo yanafanana na suala hilo na tayari yanaweka precedences. Mathalani hata sasa vipo vyama ambavyo pamoja na kuwa na uwakilishi bungeni (mbunge mmoja), ambayo ni sawa na asilimia 0.000 katika bunge la sasa, hata katika baadhi ya maamuzi yanayozingatia kanuni za namna hiyo au zinazofanana na hizo, taratibu za kisheria zilizopo zinawaweka kando katika masuala kadha wa kadha kama ruzuku au kupata wabunge wa viti maalum. Hiyo inadhihirisha kuwa vyama vikafanye kazi ya siasa kuongeza viti bungeni ili vipate au kuongeza nafasi za wagombea wa EALA watakaowakilisha nchi yetu kwenye bunge hilo.
Ni muhimu wakajua kuwa nafasi hizi za EALA kwa utaratibu uliopo sasa hazigawiwi tu kama sandakarawe au jugu ama pipi. Ni matokeo pia ya kazi kubwa iliyofanyika wakati wa kampeni uchaguzi uliopita.
Tusubiri uteuzi kuelekea uchaguzi EALA.
Tumaini Makene