KAMISHNA Jenerali wa Uhamiaji Dk Anna Makakala amefanya mabadiliko ya viongozi wa Uhamiaji wa mikoa na kuteua wapya Tanzania Bara na Visiwani.
Mabadiliko hayo yamemgusa Kamishna wa Idara hiyo Kanda ya Dar es Salaam, John Msumule ambaye ameondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Naibu Kamishna Mary Palmer.
Kwa mujibu wa taarifa ya Dk Anna,
katika mabadiliko hayo, Sixstus Nyaki aliyekuwa Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa wa Mwanza amehamishiwa Simiyu wakati aliyekuwa na nafasi kama hiyo mkoani Rukwa, Selemani Kameya amehamishiwa Tabora.
Aidha, katika mabadiliko hayo, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, Asumsio Achacha amehamishiwa mkoa wa Kaskazini Pemba huku aliyekuwa Manyara, Peter Kundy akihamishiwa Dodoma kuchukua nafasi ya Ali Mohamed ambaye amehamishiwa Arusha.
Mkemi Mhina Seif ameteuliwa kuongoza mkoa wa Kusini Unguja, huku Muhsin Abdallah Muhsin akiteuliwa kuongoza mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika mabadiliko hayo pia, Said Omary Hamdani ataongoza idara hiyo mkoa wa Mjini Magharibi na Othman Khamis Salum anakuwa Mkuu wa Uhamiaji Mjini Magharibi Unguja.
Baadhi ya wakuu wa Uhamiaji wa mikoa wamebaki kwenye vituo vyao vya kazi vya awali.
Katika mabadiliko hayo, Kamishna Jenerali Makakala pia aliteua viongozi wapya idara kwenye baadhi ya mikoa ambapo Plasid Mazengo ameteuliwa kuongoza mkoa wa Pwani huku Mrakibu Mwandamizi James Mwanjotile akipelekwa kuongoza Mtwara.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Hope Kawawa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa na Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Hosea Kagimbo anahamishiwa mkoa wa Njombe.
Wengine ni Rashid Magetta anakuwa Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa wa Songwe, Carlos Haule, anakwenda Rukwa; Julieth Sagamiko, Manyara; Albert Rwelamila, Kilimanjaro na Paul Eranga, Mwanza.
Crispin Ngonyani anakwenda Tanga; Shaban Hatibu, Katavi; Remigius Pesambili, Kigoma na Novaita Mrosso anakwenda Mbeya.
Aidha, Bakari Mohamed Ameir anakuwa Mkuu wa Kituo cha Uhamiaji cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) na Fulgence Mutarasha anakuwa Mkuu wa Uhamiaji Kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).