Kisa cha Mbuzi Wanaojichunga Wenyewe Dar, Mzee Anayewamiliki Asema Ukiiwaiba Utawarudisha Tu..!!


Kama wewe ni mtembezi mzuri wa jiji la Dar es Salaam, bila shaka umewahi kukutana na kundi la mbuzi wanaokatiza barabarani wao wenyewe bila mtu anayewachunga. 

Mbuzi hawa ni maarufu, huja mjini na kurudi wanakokaa bila kudhurika. Hakuna anayediriki kuwaiba wala kuwadhuru – waguse uone.

Mwandishi wa BBC Swahili, Humphrey Mgonja aliamua kuwafuatilia ili kubaini ukweli wa maisha yao, na aliyoyabaini, yatakuacha mdomo wazi.

“Wakifika barabarani hapo wanasimama kama vile binadamu, wanaangalia huku na huku wakiona gari hamna wanavuka, wana akili kuliko binadamu,” anasema mkazi mmoja wa Dar es Salaam.

“Wanavuka katikati ya zebra, mbuzi gani wa kuvuka katikati ya zebra kama binadamu?” Anahoji mwingine.

Kwa aliyewahi kutaka kuwafanyia hila mbuzi hao, cha moto alikiona.

“Aliwachukua Shoppers akawapeleka Vingunguti machinjioni, lakini kule hakufanikiwa hata kushika mbuzi mmoja, alichofanya ni kurudisha mbuzi hadi hapa Shoppers akainua gari lake, mbuzi wakaruka akaachana nao yeye akaamua kuondoka zake,” anasema Pascal Mshau aliyewahi kumshuhudia nduguye aliyejaribu kuwachukua.

Mwandishi Humphrey Mgonja aliwafuatilia mbuzi hao hadi usiku wa saa mbili walipoelekea kwenye makaburi ya Kinondoni ambako ndiko yalipo makazi yao. Mmiliki wa mbuzi hao, Mzee Omari amemwelezesha mwandishi huyo kuwa mbuzi wake hawaibiki.

“Hawa mbuzi huwa siwachungi, na wala huwa siwafungi, huwa nawaacha wanaenda kula wenyewe malishoni huko baada ya muda wanarudi wenyewe hapa nyumbani,” anasema mzee huyo.

“Sijawahi kuibiwa, na hata kama ataiba mtu, yeye mwenyewe atanirudishia tu, atarudisha mwenyewe,” anaongea kwa kujiamini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad