SANAMU ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Nyerere Square mjini hapa, imepata umaarufu kutokana na watu wengi kutoka maeneo mbalimbali mchini kufika na kupiga picha za kumbukumbu na sanamu hiyo.
Sanamu hiyo ya Mwalimu Nyerere ambayo Baba wa Taifa ameshika fimbo mkononi, ipo mjini Dodoma, inatumiwa na watu mbalimbali kupiga picha za kumbukumbu mbalimbali kutokana na heshima ya kiongozi huyo.
“Watu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa Dodoma na mikoa mingine wanaofika Dodoma wanakwenda mahali hapo na kupiga picha za kumbukumbu mbele ya sanamu hiyo ya Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere,” anasema Masoud Abdallah ambaye ni mpigapicha katika eneo hilo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Hilda Meada katika mazungumzo na gazeti hili, alisema eneo la Nyerere Square ambalo ni maarufu kwa wapigapicha ni miongoni mwa maeneo ambayo CDA imeyakabidhi kwa manispaa.
“Eneo hilo ambalo lilikuwa likisimamiwa na kufanyiwa ukarabati na uboreshaji na CDA na sasa limekabidhiwa kwa Manispaa ya Dodoma ambayo inajipanga kuhakikisha eneo hilo na mengine yaliyopo Dodoma yanaboreshwa na kulingana na mji huu kuwa makao makuu ya serikali,” alisema Maeda.
Alisema manispaa ina mkakati mkubwa wa kuhakikisha eneo hilo na maeneo mengine ya wazi yanafanyiwa ukarabati na uboreshaji wa kutosha ili kuendana na hadhi ya mji.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema manispaa imejipanga kikamilifu kuhakikisha maeneo yaliyokuwa ya wazi ambayo yamerudishwa kutoka CDA wanataka kuyaboresha na kuhakikisha yanakuwa sehemu ya vivutio muhimu kwa watu mbalimbali wanaotembelea likiwamo hilo na Nyerere Square.
Mpigapicha Said Juma alisema, hicho ni kituo chao kutokana na watu wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini kufika hapo na kutaka kupiga picha na sanamu ya Baba wa Taifa.
“Hapa kimekuwa kituo chetu cha kupigia picha kutokana na watu wengi wanaotoka mjini Dodoma, kuja kuweka kumbukumbu ya kuingia hapa kwa kupigia picha mahali hapa,” alisema Juma.