KOCHA msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema kuongezeka kwa majeruhi katika kikosi chao ni pigo na wataivaa kiugumu MC Alger ya Algeria katika mchezo wa Kombe la barani Afrika utakaochezwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kinakabiliwa na majeruhi wengi baada ya Mzambia Justine Zullu kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam uliochezwa juzi, Uwanja wa Taifa na wao kushinda bao 1-0.
Wachezaji wengine majeruhi ni washambuliaji Amis Tambwe, Donald Ngoma, kiungo Thabani Kamusoko na beki Pato Ngonyani.
Akizungumza juzi, Mwambusi alisema majeruhi walionao wamezidi kupunguza idadi ya wachezaji muhimu wa kikosi chao cha kwanza.
Mwambusi alisema hali hiyo imekuwa ikiwagharimu mara nyingi ukizingatia wameanza vibaya katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa mapema.
“Inasikitisha sana kuongezeka kwa majeruhi katika kikosi chetu, tunazidi kuwapunguza watu na tunakwenda kwenye michuano muhimu ambayo lengo letu ni kufanya vizuri baada ya kuanza vibaya,” alisema Mwambusi.
Mwambusi alisema malengo yao ni kutaka kufika mbali katika michuano hiyo, lakini wamekuwa wakiandamwa na majeraha na ni pigo.
Alisema wachezaji watano majeruhi ambao wanacheza kikosi cha kwanza, hivyo wanahitaji kufanya kazi kubwa kurudi katika hali ya kawaida.