Mbunge wa Kigoma mjini kwa tiketi ya Chama Cha ACT Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe amefunguka na kusema atapeleka hoja binafsi bungeni kulitaka Bunge kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utekaji, uteswaji na hata mauaji ya raia
Zitto amesema vitendo hivyo vinahusisha pia suala la kijana Ben Saanane ambaye mpaka sasa ni zaidi ya miezi sita amepotea na haijaulikana wapi alipo.
Amesema hayo jana bungeni wakati akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/18 ambapoi amesema kutoweka kwa Ben Saanane kunahusishwa na watu wa usalama wa Taifa.
"Kuna kijana wa kitanzania, ndugu Ben Saanane amepotea kwa zaidi ya miezi mitano sasa. Hajulikani alipo. Wazazi wake na rafiki zake wamemtafuta na kutoa malalamiko bila mafanikio. Wamefikisha taarifa kwa jeshi la polisi na wamepaza sauti bila kuchoka. Kuna nyakati suala hili lilionekana la siasa na ndiyo maana wengine tulikaa pembeni. Lakini sasa ni miezi 6, hakuna taarifa juu ya suala hili, nimeona nisikae kimya juu ya hili. Taarifa zinatoka chini chini, siyo rasmi, kwamba huyu kijana 'ametoweshwa'. Kwamba alishikiliwa na watu wa Idara ya Usalama na amepotezwa. Jeshi la Polisi wana taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben Saanane kwa kutumia simu yake ya mkononi, ambayo inaonekana simu ilipoteza mawasiliano akiwa maeneo ya Buguruni siku aliyotekwa tarehe 15/16 Novemba 2016 na tangu siku hiyo hapakuwa na mawasiliano tena." alisema Ziito Kabwe .
Mbunge Zitto Kabwe anasema kuwa matukio ya utekwaji, uteswaji yamekuwa yakitokea tangu huko nyuma lakini polisi wamekuwa wakikaa kimya na mpaka leo hakuna hata mmoja ambaye alikamatwa kuhusiana na mambo hayo.
"Kumekuwa na matukio ya namna hii mabaya kabisa huko nyuma; ndugu Absalom Kibanda,
aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri alivamiwa na kuumizwa vibaya sana na leo jicho lake moja halioni mwaka 2013. Pia ndugu Yona wa Temeke alitekwa na kuumizwa na kutupwa huko Mbweni jijini Dar es salaam na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa juu ya matukio yote hayo. Orodha ya matukio ya namna hii ni ndefu. Watanzania wamesahaulishwa yote haya, Polisi mpaka leo hawajamkata hata mtu mmoja juu ya yote hayo". Alisema Zitto
Kutokana na mambo haya Zitto Kabwe amekusudia kupeleka hoja binafsi bungeni ili bunge liweze kuunda kamati na kuchunguza mambo hayo ambayo anasema yanaleta chuki dhidi ya wananchi na taasisi ya TISS.
"Mambo haya maovu yanayohusishwa na Idara hii yanaondoa uhalali wa Taasisi hii kwa wananchi, yanaondoa heshima, hadhi na uaminifu juu ya idara hii, yanajenga chuki na taswira hasi ya Wananchi kwa idara hii, hili si jambo jema kwa taifa. Ni wakati sasa wa kuchukua hatua.
Ni lazima Bunge liamke na kukomesha hali hii. Kwa mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Bunge natoa taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utekaji, uteswaji na hata mauaji dhidi ya raia (suala la Ben Saanane likiwemo)" alisema Zitto Kabwe