AKIWA mwalimu wa shule ya msingi na mwanamitindo, Harnaam Kaur aliingia katika Kitabu cha Rekodi za Dunia (Guinness World Records) kuwa mwanamke mdogo duniani mwenye ndevu nyingi zaidi.
Kaur (24), aliweza kukabiliana na changamoto za miaka mingi za hali aliyo nayo ikiwamo kejeri, kebehi, zomea zomea na kila aina ya maneno mabaya hadi kufanikiwa kujiamini na kukomaa na nywele zake hizo za usoni.
Aliingia katika rekodi hizo kwa ndevu zake za inchi sita ikiwa ni matokeo ya kusitisha mpango wa kuzikata.
Mkazi huyo wa mji wa Slough, Kusini Mashariki mwa Uingereza pia amewahi kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu asiowafahamu mitandaoni.
Kisa cha kumtishia ni ndevu zake nyingi zinazomfanya asitofautishwe kirahisi na mwanamume.
Mwanamke huyo ana tatizo la homoni linalomfanya kuwa na vinyweleo vingi kupita kiasi likijulikana kitaalamu kama ‘polycystic ovary syndrome.’
Ameeleza alianza kupata tatizo hilo akiwa na umri wa miaka 11 na alikuwa akizinyoa mara mbili kwa wiki.
Awali mwanadada huyo alikuwa akijitahidi kuzipunguza na kunyoa lakini ilishindikana, sasa ameamua kujiamini jinsi alivyo, ingawa vijana wa rika lake humuona kama mtu wa ajabu.
Ameeleza kuwa alipokuwa shuleni alikuwa akionewa kwa kuitwa majina mengi ya kejeli kama ‘jike dume’, na alishindwa hata kuwaangalia watu usoni.
Alipotoka shule, alienda moja kwa moja nyumbani na kujifungia humo siku zote asionekane mara kwa mara.
Anaongeza kuwa kutokana na kuishi katika hali hiyo alifikia hatua ya kutaka kujiua.
“Wakati nimekaa na kupanga kujiua, nilianza kujishauri, nilijiambia: 'Nguvu unayotumia kuhitimisha maisha yako, kwanini usiitumie kugeuza maisha yako na kufanya kitu kilicho bora?”
Na hivyo, akaamua kujiunga na dini ya Singasinga, Imani ambayo hairuhusu watu kunyoa vinyweleo vyao kwa kuwa Mungu ndiye aliyewaumba hivyo.
“Wakati nilipoanza kuacha nywele zikue ilikuwa sababu za kidini, lakini kwa kadiri miaka ilivyosonga mbele, sababu nyingine kuu zaidi ni kwamba napenda jinsi nilivyo”, alisema wakati wa mahojiano baada ya picha yake kutumikla katika maonesho ya kusherehekea watu wenye ndevu bora duniani.
Kwa hiyo ameziachia nywele zake na sasa anaonekana kama mwanaume akiwa na nywele nyingi kidevuni, mikononi na kifuani.
Uamuzi wake awali uliikanganya hasa familia yake, ambayo Kaur anasema: “Mama na baba yangu hawakufurahia uamuzi huo kwa vile walikuwa wana wasiwasi nisingeweza kuishi maisha ya kawaida iwapo ningekuwa na ndevu.
“Walikuwa na wasiwasi kwamba nisingeweza kuolewa wala kupata ajira. Lakini nilitaka kusimamia na uamuzi wangu kwa ajili yangu na si mtu mwingine. Awali niliishi kwa kujificha na kuumia vya kutosha. Hiyo ilitosha!”
Wazazi wake sasa wameukubali uamuzi wake huo na kaka yake Gurdeep Singh (18) ni shabiki wake namba moja.
Kaka yangu ni kweli alikuwa mmoja wa watu aliyeshtushwa na uamuzi wangu wa kutonyoa, lakini alinikumbatia na kunieleza kwamba naonekana mrembo zaidi niwapo na ndevu, lakini hakufahamu kwanini niliamua vile.’
Aliongeza: “maneno haya ya kaka yalitosha kunifanya nikomae na ndevu zangu.’
Anasema: “tangu aamue kujikita na nywele usoni, watu walizidisha kiwango cha kumkazia macho. Awali nilikuwa na hasira, lakini nilitambua hawakufahamu na ni wazi wanaogopa kuniuliza na hivyo huamua kurudisha tabasamu kwao.”
Anaihesabu hiyo kama ‘heshima’ na kwamba itasaidia kuchochea wanawake wengine kujikubali walivyo au wanavyotaka kuwa.
Imani hiyo imempa ujasiri zaidi juu ya muonekano wake, na anajiona mwanamke mwenye mvuto zaidi.
“Nahisi nimekuwa mwanamke zaidi, nina mvuto zaidi na nadhani naonekana hivyo pia. Nimejifunza kupenda jinsi nilivyo na hakuna kitakachonitikisa sasa hivi,” anasema Harnaam.
“Naweza kwenda kwenye maduka ya wanawake bila kuhisi kuwa sitakiwi kuwa kule. Navaa sketi, gauni na vidani na napenda kutengeneza kucha zangu kama msichana mwingine yeyote.”
Machi mwaka jana alikuwa mwanamke wa kwanza mwenye ndevu kushiriki maonesho ya mitindo ya London.
Amekuwa akipokea dili ikiwamo kupamba majarida mbalimbali ya mavazi ikiwamo kupiga picha akiwa katika mavazi ya harusi.
Akiwa na furaha sasa Kaur ameajiriwa kama msaidizi wa walimu katika Shule ya Msingi ya Singasinga na kumfanya imani yake ipae.
Anasema wauza duka shuleni humuita ‘bwana’ na kwamba watu wengine huniangalia kwanza wakionan ndevu kisha wanaposhusha macho chini wanabaini nina matiti pia. Inakanganya watu wengi hakika!.
“Kichekesho zaidi ni kutoka kwa watoto katika shule yangu. Baadhi huniuliza ndevu zangu ni nini. Nawajibu ni vinyango vya vibwengo. Baadhi huniuliza nanunua wapi na huwajibu tu ‘Asda”.