RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema Bunge linalazimika kuunda tume ya kuchunguza walinzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Alisema hayo katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii jana akibainisha kuwa iwapo mlinzi aliyemtisha kwa bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ni kosa kisheria.
“Nimeona taarifa kwamba mtu aliyemtolea Nape bastola majuzi ni mlinzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni ofisa wa TISS, kama taarifa hizi ni za kweli, basi mtu huyo anapaswa kufukuzwa kazi mara moja, kukamatwa na kushitakiwa kijinai,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha TISS, maofisa usalama wa taifa wamekatazwa kufanya kazi za kipolisi kama kukamata wahalifu, kuhoji watuhumiwa na kufanya upelelezi wa kijinai.
Lissu alisema alichokifanya kumzuia Nape kuzungumza na waandishi wa habari kwa kumtishia bastola kinaangukia majukumu ya kipolisi ambayo TISS haina mamlaka nayo kwa mujibu wa sheria.
“Kikubwa na muhimu zaidi ni hiki: huyu askari wa TISS alikuwa anafanya kazi kwa maagizo au maelekezo au amri ya nani?” Alihoji.
Rais huyo wa TLS alisema kama alikuwa anatekeleza maagizo ya bosi wake yaani Mkuu wa Mkoa au bosi mwingine, hao nao wanapaswa kufukuzwa kazi na kushitakiwa kijinai.
Mbunge huyo alisema kama ni maagizo ya Rais John Magufuli kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, basi hiyo ni fursa ya mashitaka ya Bunge dhidi ya Rais.
Alisema jambo hilo ni kubwa linalohitaji kuundiwa kamati teule ya Bunge kulichunguza na kuchunguza mazingira yote yanayomzunguka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na matumizi yake ya askari wa vikosi vya ulinzi na usalama.
Lissu alisema Mkuu wa Mkoa huyo anaelekea kuamini kwamba ana uwezo wa kutumia askari atakavyo yeye binafsi.
“Anatakiwa kuondolewa mawazo hayo ya kijinga kabla hajafanya jambo kubwa na baya zaidi,” alisema.