Msanii wa muziki wa hip hop ambaye aliyekua katika Kundi la Weusi, Lord Eyes, amefunguka mengi kuhusu kundi hilo baada ya kuonekana kufanya kazi peke yake.
Kundi hilo ambalo lilikuwa likiundwa na wasanii 5, Joh Makini, Nikki wa Pili, G Nako, Bonta pamoja na Lord Eyes, limebaki na wasanii watatu tu ambao ni Joh Makini, Nikki wa Pili na G Nako pekee.
Akiongea katika kipindi cha XXL cha Clouds FM wiki hii, Lord Eyes amesikika akidai kundi hilo limejaa utengano, ubinafsi na wivu.
“Hatujawahi kuwa kwenye crew,” alisema Lord “Tuliungana kutanua wigo lakini sio kwa mkataba wala chochote. Weusi ni kampuni. Watu wanasema kila siku, ni kundi lakini ni kampuni, na ndio maana kumekuwa na utengano, ubinafsi na wivu,”
Pia rapa huyo alisema kila msanii wa kundi hilo anamiliki hisa za asilimia 20 ya kampuni hiyo.
“Kuna maceo watano ndani ya Weusi na kila mtu alikuwa ana share yake, yaani asilimia 20 kila mmoja. Hii asilimia 20 kila mtu ameifanyia kazi, kwa sababu wigo ambao tulitaka kutanua ni kwenda mbele zaidi, tuwe na nguvu kwani umoja ni nguvu, lakini haikuwa hivyo. Imekuwa kama Weusi ya River Camp,” alisema Lord.
Lord Eyez pia aliachia wimbo wake mpya ‘Hela Yangu’, aliyoifanya chini ya msaada wa Barakah The Prince.