Mastaa Watano wa Kike Tanzania Wanaopeta Kwenye Muziki Bila Kiki

MASTAA WATANO WA KIKE TANZANIA WANAOPETA KWENYE MUZIKI BILA KIKI

Muziki wa Tanzania umekuwa kwa kiasi kikubwa mpaka kufikia wasanii kadha wa kadha kufanya kazi za muziki wakishirikiana na wasanii maarufu kutoka nje ya nchi.

Pamoja na kukua kwa muziki wa Tanzania, bado wapo wasanii wanaopenda kusikika kwenya vyombo vya habari na kurasa za magazeti hata kama hawana kazi zenye kuvutia kwa wakati huo.

Suala la kupenda kuonekana ‘kideoni’ na kuzungumziwa na watu wengi tunalifahamu kwa jina moja ‘KIKI’. Baadhi ya wasanii wamediriki hata kufanya mambo ya kujidhalilisha ilimradi tu wapate ‘kiki’ mitandaoni.

‘Kiki’ imekuwa ikisakwa sana na wasanii hasa wale wa kike ili waendelee kusikika na kukaa kwenye chati ya muziki nchini na hata nje ya nchi.

Lakini hili limekuwa tofauti kwa baadhi ya wasanii hapa nchini kwani wao wameamua kuendesha kazi zao za sanaa bila kutegemea ‘Kiki’ za mitandaoni na kwenye magazeti.

Kwa wasanii wa kike kukaa bila kuwa na ‘kiki’ au ‘skendo’ ni nadra sana, lakini nakuhakikishia hawa wamejitahidi kuweka rekodi ya kutokutegemea mambo hayo katika sanaa zao.

MAUA SAMA 


Huyu ni mwimbaji hodari wa nyimbo za mapenzi, ana sauti nyororo anayoitumia vyema kuumudu ushindani uliopo kwenye Bongo Fleva. Anamiliki hit Song kama ‘So Crazy’, ‘Let them Know’, ‘Sisikii’, ‘Mahaba Niue’ na ‘Main Chick’.

Zaidi ya muziki wake kumfanya ajulikane katika ulimwengu wa Bongofleva mpaka kuchukua tuzo ya Wimbo Bora wa Raggae- Let Them Know, hajawahi kufikiria kutengeneza tukio la kumpa kiki katika kazi zake.

NANDY



Mrembo huyu ni balozi wa taasisi iliyoanzishwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson. Heshima ambayo imekuja baada ya kuonekana msafi ambaye hana makandokando kwenye maisha ya ustaa. Ubalozi ni dili ambalo wasanii wengi wa kike wamelikosa kutokana na skendo au kiki ambazo mwisho wa siku zimeondoa heshima yao.

Nandy amekuwa staa kutokana na mashabiki kumpa usikivu kupitia nyimbo zake kama ‘Nagusagusa’ na ‘One Day’.

ROSA REE



Kutoka The Industry, lebo inayomilikiwa na Kundi la Navy kenzo tunakutana na rapa mwenye sauti na michano yenye mamlaka Rosa Ree ambaye hivi karibuni aliungana na Rick Ross katika dili la ubalozi wa kinywaji cha Luc Baraile.

Kiki siyo sehemu ya maisha yake sababu uwezo wake wa kuchana pekee ni kiki tosha kwenye muziki wa Hip Hop kiasi kwamba rapa mkubwa kama Joh Makini amemtabiria makubwa huko mbeleni.

MIMI MARS



Anaitwa Marianne Mdee ambaye ni mdogo wa damu na Vanessa Mdee. Ni mtangazaji ambaye amejiongeza kwa kutumia talanta yake ya pili ya uimbaji na sasa anasumbua na ngoma inayoitwa Shuga.

Hapendi sana kutumia mgongo wa dada yake ili kufika kwenye kilele cha mafanikio. Anatambua kiki siyo afya kwa uhai wa muziki wake ndiyo maana amekaza kwa kufanya kazi nzuri zilizompa mashabiki wa kutosha.

CHEMICAL


Ni nadra msichana mdogo kujiamini kiasi kile, rapa Chemical ni alama ya warembo wote wenye ujasiri wa kukabili hali zote zilizopo kwenye muziki wa Bongo Fleva. Ni muwazi na mkweli, asiyependa kupindisha mambo. Hajawahi kutumia kiki ili kusukuma ngoma zake. Skendo pia huwa anazikwepa kwa sababu hataki kuzichanganya na muziki alioujenga kwa miaka mitatu sasa.

Mfano kipindi kile msanii Stereo alipotangaza hadharani kumpenda, Chemical aliutatua msala ule bila kuacha madhara kwenye muziki wake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad