Mshtakiwa Paulo Mdonondo anayetuhumiwa na wenzake 6 kumuua aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Dkt. Sengondo mvungi, anadai alishiriki katika tukio na alilipwa ujira wa Sh 30,000 kwa kazi aliyofanya.
Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati Wakili wa Jamhuri, Patrick Mwita aliposoma ushahidi wa mashahidi 30 wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo Mahakama Kuu.
Mwita alidai mshtakiwa Paulo alipohojiwa Polisi, alikiri kushiriki katika tukio hilo na kwamba kazi yake ilikuwa kulinda majirani wasifike kutoa msaada kwa Dkt. Mvungi wakati uvamizi ukifanyika.
Inadaiwa mshtakiwa huyo alikaa nje akiwa na mawe kuzuia majirani, alifanikiwa na akalipwa Sh 30,000 na tukio lilipomalizika alienda kupanda daladala kuelekea katika shughuli zake Kariakoo.
Chanzo: Mtanzania