Macho na masikio ya wadau wote wa soka yatakuwa kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji inayokutana leo kupitia hukumu ya Kamati ya Saa 72 iliyowapa pointi za chee Simba.
Simba inaomba Mungu uamuzi wa Kamati ya saa 72 uendelee kubaki kama ulivyo ili pointi zake zisipunguzwe na iendelee kuwa na matumaini ya ubingwa msimu huu wakati Yanga inaomba Kagera Sugar irejeshewe pointi zake ili iwe kazi rahisi kwao kutetea ubingwa wao.
Kamati ya Saa 72 wiki iliyopita iliipoka pointi Kagera Sugar na kuipa Simba kwa madai ilimchezesha beki Mohammed Fakhi aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Simba ilidai Fakhi alicheza dhidi yao wakati Kagera ikipata ushindi wa mabao 2-1, huku akiwa na kadi tatu za njano alizopata katika mchezo dhidi ya Mbeya City, African Lyon na Majimaji.
Jambo hilo limepingwa na Kagera Sugar na kuamua kukata rufani Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) wakiomba uamuzi wa Kamati ya Saa 72 upitiwe upya kwani wao wana ushahidi kuwa beki wao Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano.
Tayari Kagera imetuma ujumbe wa watu watatu kuhudhuria kikao hicho na kushusha ushahidi wao na mmoja wao ni mtuhumiwa Mohammed Fakhi, meneja wa timu Mohammed Hussein na kocha wa makipa, Mussa Mbaya.
Watu wengine waliotajwa kuhudhuria kikao hicho ni kutoka bodi ya ligi, Joel Balisidya, Rose Msamila, Michael Ngogo, wasimamizi wote wa mchezo kati ya Kagera Sugar na African Lyon wakiwemo waamuzi na kamisaa wa mchezo huo.
Meneja wa Kagera Sugar, Hussein alisema anaamini haki itetendeka na watarejeshewa pointi zao.
“Mchezaji wetu hakuwa na kadi tatu za njano siku hiyo na ushahidi wa kila kitu tumekuja nao na tutauwasilisha kwa kamati.”