IMEELEZWA kuwa, askari wanaopoteza maisha wakiwa katika vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na Serikali ya Tanzania kupitia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) hutoa fidia kwa ndugu zao walio hai.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Malindi, Ally Saleh Ally (CUF) aliyetaka kujua kama kuna fidia kwa ndugu wa askari wanaokufa wakiwa vitani au katika kulinda amani.
“Askari wanaopoteza maisha wakiwa katika kulinda amani, Umoja wa Mataifa na JWTZ hutoa fidia kwa familia husika ili ziendelee kuishi baada ya ndugu yao kufariki dunia,” alisema.
Akijibu swali la msingi la Mbunge Ally aliyetaka kujua kama mazoezi ya vikosi vya kulinda amani yanaimarisha jina la Tanzania kiasi gani, Dk Mwinyi alisema, ushiriki wa Tanzania katika kulinda amani Afrika unailetea nchi heshima kubwa duniani.
“Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na inatimiza wajibu wake wa kuzisaidia nchi zenye migogoro ili kuleta amani, ushiriki huo unaleta heshima kubwa duniani,” alisema.
Alisema heshima kubwa inaletwa kutokana na ushiriki huo wa Tanzania na utayari wake wa kutoa misaada ya ulinzi wa amani na kazi nzuri inayofanywa na jeshi.
Alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania ilipeleka vikosi vya ulinzi wa amani kombania mbili nchini Lebanon tangu mwaka 2008 na ilipeleka Darfur, Sudan kikosi kimoja tangu 2009.
“Tanzania pia ilipeleka vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zaidi ya kikosi kimoja chenye watu 1,256 tangu mwaka 2013,” alisema na kuongeza kuwa, kila kikundi hufanya jukumu la ulinzi wa amani kwa muda wa mwaka mmoja na kubadilishwa.
Katika kukusanya vikundi kabla ya kupelekwa nje ya nchi kwenye majukumu hayo, alisema changamoto zinazojitokeza ni gharama za kuandaa za kuvihudumia vikosi hivyo vikiwa kwenye mafunzo.
“Pia gharama za vifaa vya wanajeshi vitakavyotumika katika eneo la uwajibikaji na ugumu wa kupata mafunzo ya uhalisia wa maeneo wanayokwenda kwa mfano jangwani au misituni,” alisema.