Kufuatia watu wanane kuibuka wakiwa na silaha na kusababisha vurugu kwenye mkutano wa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya kinondoni, Dar, Jumamosi iliyopita, Mbunge wa Mtama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Moses Nnauye ametia neno kwa kusema kuwa hizo ni siasa za kinung’ayembe.
Jana Nape aliandika kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Twitter: “Siasa ni ushindani wa hoja na siyo nguvu! Tunakwenda wapi huku jamani? Wanavamia na kutoroka!!?? How!!? Siasa imevamiwa na manung’anyembe sasa!
Tafsiri ya nung’ayembe ni mwanamke asiyeolewa anayehangaika ya maisha ya kurukaruka.
Tukio la kufanyiwa fujo mkutano wa CUF lilijiri katika Hoteli ya Niva iliyopo Mabibo, Dar ambapo ilidaiwa kuwa, wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Maalim Seif waliumizwa kwa kupigwa na wavamizi waliodaiwa ni wale wanamuunga mkono Profesa Lipumba.
Katika vurugu hizo, pia wandishi wa habari ambao walijitete lakini walishambuliwa ni pamoja na Fred Mwanjala wa Channel Ten ambaye aliharibiwa kamera yake, Merry Geofrey (Nipashe) aliyeumia sehemu ya mkono na kushonwa nyuzi mbili, Rachel Chizoza (Clouds FM), Kalunde Jamal (Mwananchi), Henry Mwang’onde (The Guardian), Mariam Mziwanda (Uhuru), Estherbella Malisa (Azam TV) na Asha Bani (Mtanzania).