Ni Mwendo wa Kuisoma Namba Tuu..Wabunge Nao Walio Kutolipwa Posho na Mishahara kwa Wakati..Wadai Siku Hizi Kwenye Vikaoa Wanalishwa Chai na Viazi vya Kuchemsha..!!!


NI kilio! Hivyo ndivyo inavyoelezwa kuhusiana na hali ya ukata inayolikabili Bunge la Tanzania na kuwalazimu baadhi ya wabunge kubadili mtindo wa maisha mjini Dodoma.


Uchunguzi uliofanywa na Nipashe na kuwahoji wabunge mbalimbali, umebaini kuwa kupungua kwa fedha zinazopaswa kutolewa kwa chombo hicho pamoja na utekelezaji wa hatua mbalimbali za kubana matumizi kumesababisha baadhi ya wabunge kuachana na magari ya kifahari waliyokuwa wakiyatumia wakiwa kwenye vikao vya bunge mjini hapa na kusafiri kwa mabasi kutoka majimboni.

Pia imebainika kuwa athari nyingine kwa wabunge ni pamoja na baadhi kuhama vyumba vya hoteli za bei mbaya na kwenda kuishi kwenye nyumba za wageni za bei nafuu; kubadili sehemu za kupata milo ya kila uchao na kupungua idadi ya wageni wanaoletwa na wabunge kupitia ziara za wapigakura wao wakiwamo madiwani wa majimbo yao.

Hatua hiyo pia imesababisha kupungua kwa fedha kwa wabunge kulinganisha na miaka iliyopita hivyo kuwafanya kuwa katika hali ngumu ya kurejesha mikopo ambayo baadhi waliichangamkia kwa kuamini watailipa kirahisi kutokana na posho mbalimbali.

“Kuna wakati hata posho zilizopo hazipatikani kwa wakati. Matokeo yake, wabunge wengi hivi sasa wamelazimika kuwa wagumu wa kutoa fedha kusaidia mambo mbalimbali majimboni,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe na kukumbushia baadhi ya wabunge walivyokuwa wakitaniwa majimboni mwao kuitwa ATM (mashine za kutolea fedha za kielektroniki), lakini sasa jina hilo halipo kwa sababu wengi hutegemea fedha za Mfuko wa Jimbo pekee.

“Mambo yamekuwa magumu. Wakati mwingine fedha hazipatikani kwa namna iliyozoeleka miaka ya nyuma,” chanzo kiliongeza.

Imedaiwa kuwa hali hiyo ngumu kifedha imetokana na serikali kushindwa kutoa fedha zilizopitishwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, alifichua namna Bunge lilivyo na hali ngumu kifedha kiasi cha kutishia shughuli zake katika vikao vinavyoendelea vya Bunge la Bajeti.

Aliitaka Serikali itoe fedha kiasi zaidi ya Sh. bilioni 21 ili kuwezesha shughuli za Bunge kuendelea. Pia fedha nyingine zaidi ya Sh. bilioni nane zitokanazo na posho mbalimbali za wabunge.

waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliliambia Bunge Machi 28, mwaka huu, kuwa utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha umekuwa wa kusuasua kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na mwamko mdogo wa Watanzania kulipa kodi na pia sehemu ya fedha kuelekezwa katika kulipia madeni.

Sababu nyingine ni kuchelewa kutolewa kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu; riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha la kimataifa kuwa juu na pia matayarisho hafifu ya miradi.

WABUNGE ZAIDI WAFUNGUKA
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), alisema ukata unaolikabili Bunge umetokana na kitendo cha serikali kupanga bajeti ya mfuko wa chombo hicho bila kuzingatia uhalisia.

Hasunga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), aliishauri serikali kutenga nyongeza ya bajeti kulinusuru Bunge ambalo pia linakabiliwa na madeni ya mabilioni ya shilingi.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema hali ya kifedha ni mbaya huku akidai si kwa chombo hicho tu bali ofisi mbalimbali za serikali kutokana na utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu kuwa chini ya asilimia 40.

Alisema moja ya athari ambazo sasa wabunge wanazipata kutokana na hali hiyo ni kukosa fedha na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Lema alisema kukauka kwa fedha mifukoni mwa wabunge kumetokana na Bunge kushindwa kuwalipa mishahara na posho zao kwa wakati.

"Hata kwenye kamati sasa ni chai, kiazi na andazi tu….kula vizuri, kuishi vizuri kwa class si kufuja. Ndiyo maisha ya binadamu. Na hii si kwa wabunge tu, inatakiwa kwa Watanzania wote ndiyo maana tunapigania maisha bora kwa kila Mtanzania,” alisema Lema, akifichua vilevile kuwa baadhi ya wabunge sasa wamelazimika kuacha magari yao na kupanda mabasi.

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), aliimbia Nipashe mjini hapa jana kuwa kutokana na ukata uliopo, shughuli za Bunge zinaendea kwa kusuasua na kuungana na Hasunga na Lema kuthibitisha kuwa wabunge sasa hawalipwi mishahara na posho kwa wakati.

"Ndani ya Bunge hata vitu vidogo vidogo vyenyewe hakuna. Kuna semina za kuwajenga wabunge nazo sasa hazipo. Hata ukienda maktaba, unakosa hata magazeti kutokana na ukata. Pesa iliyokuwa imeombwa inapokosekana, kunakuwa na mazingira magumu ya kufanya kazi,” alisema Sakaya.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), mbali na kulalamika kuhusu kunyimwa safari za nje, alisema hali ya ukata bungeni inadhihirishwa na kukosekana hata kwa maji ya kutosha kwenye vikao vya kibunge.

HALI ILIVYO KIBAJETI
Kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Bajeti, katika mwaka huu wa fedha (2016/17), Mfuko wa Bunge (Fungu 42) uliidhinishiwa jumla ya Sh. bilioni 99.066. Kati yake, Sh. bilioni 23.799 ni kwa ajili ya mishahara, Sh. bilioni 68.268 ni za matumizi mengine na Sh. bilioni saba ni kwa ajili ya maendeleo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia, aliliambia Bunge mjini hapa Alhamisi kuwa hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, Ofisi ya Bunge ilikuwa imepokea Sh. bilioni 77.479. Kati yake, Sh. bilioni 59.929 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh. bilioni 17.479 kwa ajili ya mishahara.

"Hata hivyo, pamoja na kupokea fedha hizo, bado kunaonekana kuna changamoto kubwa ya kutolewa fedha kwa wakati kwa fungu husika na hivyo kuathiri utekelezaji wa baadhi ya majukumu ya Mfuko wa Bunge," alisema Ghasia.

Alisema hadi sasa mfuko huo una bakaa ya bajeti ya matumizi mengineyo ya kiasi cha Sh. bilioni 8.338 kulingana na bajeti iliyoidhinishwa.

Hata hivyo, Ghasia alisema bakaa hiyo ya bajeti haitoshi kutekeleza shughuli zilizobaki katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.

Alisema kamati yake imebaini mfuko una upungufu wa Sh. bilioni 21.196 ambao utaathiri utekelezaji wa shughuli za Bunge kwa kipindi cha robo ya nne.

Alisema matumaini ya kutatua changamoto hiyo yapo kwa kuwa kikao chao cha mashauriano na serikali, wamekubaliana upatikanaji wa bajeti ya nyongeza itafanyiwa kazi kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Ghasia ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), alisema kamati yake imethibitisha kuwapo kwa changamoto ya mgawo wa fedha kutoka Hazina kutoendana na ratiba ya shughuli za ofisi hivyo, Ofisi ya Bunge imejikuta ikiingia katika madeni ya kiasi cha Sh. bilioni 5.7.

Alisema kati ya Sh. bilioni saba zilizoidhinishwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya Mfuko wa Bunge, kamati yake imebaini kuwa ni Sh. milioni 234.09 zilizotolewa hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, sawa na asilimia tatu ya bajeti yote ya maendeleo ya ofisi hiyo.
Tags

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mbio za sakafuni huishia ukingoni"Ubunge mliugeuza kuwa"dili heavy"la kupatia pesa kiurahisi bila ya ku-sweat mwezi mmoja tu kama mbunge tayari mtu ana gari la kifahari ghorofa la kifahari pesa za kumwaga na matusi kibao kwa hao waliowachagueni muwe wabunge hamuwasaidii wananchi wenu lolote lile zaidi ya kupiga makelele yenu for nothing bungeni sasa na nyinyi imefika time yenu ya kula supu ya jiwe kudadeki zenu na bla bla zenu za uongo nkumbuke kuwa"What goes around comes around"it may take time but it will happen one day na sasa time yenu imewadia kiboko yenu Magufuli big up his Excellency Dr.Magufuli

    ReplyDelete
  2. kwani walienda kuchuma au kufanya kazi. baada ya kuwafanyia kwa waliowachagua maendeleo.wanawaza kushibisha matumbo yao. heeee!!!! hawa vip. hapa kazi tu

    ReplyDelete
  3. hapa kazi tu kula vizuri nyumbani kwako hata sisi huku maofisini tunakula hivyohivyo na bado tunachapa kazi na hatujawahi kulalamika

    ReplyDelete
  4. Takadiri Kitete na Win Rose mnaupeo mzuri sio huyo Lucy Mollely inaonekana anajazba la kuongea bila kubalance statement..km nchi aliikuta muflis na madeni ya kutupa...BIG UP MAGU,MAGU OYEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad