Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, jana wameshiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la Azania Front na kuwataka Watanzania kudumisha upendo na amani.
Pia, viongozi hao walionyesha kusikitishwa na vifo vya polisi wanane na kuitaka jamii kulisaidia jeshi hilo liweze kupambana na uhalifu.
Alhamisi iliyopita, polisi wanane waliuawa na watu wasiofahamika katika eneo la Jaribu wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Akizungumza jana mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika kanisa hilo, Lowassa alisema tukio hilo ni la kutisha na kusikitisha.
“Natoa pole kutokana na vifo vya askari polisi vilivyotokea hivi karibuni lakini nawaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwabaini waliofanya uhalifu huo,” alisema.
Alisema Polisi wasikatishwe tamaa na vitendo hivyo vya kihalifu bali wajiimarishe ili waweze kukabiliana na uhalifu kwa kuwashirikisha wananchi.
Akitoa ujumbe wa Pasaka, Lowassa aliwataka wananchi kudumisha upendo na amani kama ambavyo mafundisho ya dini zote yamekuwa yakielekeza.
“Tusherehekee Sikukuu ya Pasaka kwa upendo na amani,” alisema.
Akizungumza mara baada ya ibada hiyo, IGP Mangu aliwataka wananchi kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa amani na utulivu huku akiwahakikishia usalama wa kutosha.
“Tumeimarisha ulinzi wananchi wasiwe na wasiwasi washerehekee sikukuu hizi wakifahamu kuwa tuko pamoja nao,” alisema.
Hata hivyo, Mangu alisema wananchi bado wana mchango mkubwa kulisaidia Jeshi la Polisi kukabiliana na uhalifu kwa kutoa taarifa.
“Wananchi wema ni wengi kuliko wahalifu. Tushirikiane na Jeshi la Polisi kukabiliana na vitendo vya kihalifu kwa kutoa taarifa zinazohusu mienendo ya watu tunaowatilia shaka,” alisema.
Waziri mkuu aliyetumika kwa miaka yote kumi katika Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, aliwataka wananchi kuishi bila kubaguana na kudumisha upendo.
“Wakati tukisherehekea sikukuu ya Pasaka naomba niwaase wananchi kuishi kwa upendo, tusibaguane na tuimarishe mshikamano wetu,” alisema.
Alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuwaunganisha wananchi ili waishi kwa kushirikiana.