Noma Sana ..Rais Magufuli Akomalia Sakata la Mchanga....Hii Ndiyo Amri Mpya Aliyoitoa..!!!


RAIS John Magufuli amekazia msimamo wake wa kutaka kujua kila kilichomo kwenye makontena ya mchanga wa dhahabu baada ya kuwataka wajumbe wa kamati maalumu aliyounda kutumia utaalamu wao wote katika kupata ukweli bila kuyumbishwa na mtu.

Rais Magufuli (JPM) alitoa maelekezo hayo Ikulu jijini Dar es Salaam, jana, wakati akiwaapisha wajumbe hao wa kamati maalumu aliyounda kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini ulio ndani ya makontena yaliyoko katika maeneo mbalimbali nchini.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa hafla ya kiapo kwa wajumbe wa kamati hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju;

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi; Kamishna wa Maadili, Jaji Harold Nsekela na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa Rais alitoa maelekezo hayo baada ya kuwaapisha, akisema kuwa ameamua kuunda kamati hiyo yenye wasomi waliobobea katika masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi ili wawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50 ambao wanataka kujua ukweli kuhusu rasilimali yao ya madini.

“Hivi sasa duniani kuna vita nyingi na vita mojawapo ni vita ya uchumi, kwa hiyo tunawatuma nyinyi mwende mkapigane vita hii katika sekta hii ya madini, mkawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50, mkapate ukweli wote na wala msikubali kuyumbishwa na mtu yeyote,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Tumieni utaalamu wenu, busara zenu, uzalendo wenu kwa Taifa na upendo wenu kwa Watanzania hasa masikini wenye shida nyingi.”

Kamati hiyo ya wanasayansi wanane iliteuliwa na Rais Magufuli Machi 29 na inaongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Abdulkarim Hamis Mruma. Itafanya kazi ya uchunguzi kwa siku 20 kabla kuwasilisha ripoti yake kwa Rais.

Aidha, Rais Magufuli aliwahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kwao ili kufanikisha kazi hiyo na ametaka wawe huru kutumia vitendea kazi vyovyote vinavyohitajika, ikiwamo maabara mbalimbali za taasisi za Serikali na nyinginezo.

“Nendeni popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa ushirikiano, fungueni makontena popote yalipo, chukueni sampuli na mkazipime mjue kilichomo na naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna mtu atakayewakwamisha,” alisema Rais Magufuli.

WACHUMI, WANASHERIA PIA KUCHUNGUZA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema baada ya kuunda kamati hiyo ya wanasayansi, ataunda kamati nyingine ya wachumi na wanasheria kwa ajili ya kufanya tathmini na kuiangalia sera na sheria ya madini kwa lengo la kupata taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam na kukuta makontena 20 ya mchanga wa dhahabu yaliyokuwa tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Siku chache baadaye, yalibainika makontena mengine 262 yenye mchanga wa dhahabu yakiwa yamehifadhiwa baada ya kufuata taratibu zote za kuyasafirisha kwenda nje.

Uongozi wa Mgodi wa Acacia wenye sehemu kubwa ya makontena hayo yaliyoko bandarini Dar es Salaam ulitoa ufafanuzi kuwa makontena hayo yalifikishwa baada ya mchakato wake kufanyika kabla ya agizo la Rais kuzuia usafirishaji wa mchanga aina hiyo kwenda nje ya nchi.

KIONGOZI WA KIHINDU

Wakati huo huo, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Kihindu ya BAPS Swaminarayan Sanstha Duniani, Mtukufu Mahant Swami Maharaj ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 7.

Pamoja na kumshukuru kwa ujio wake nchini, Rais Magufuli alimhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Jumuiya hiyo na amewaalika wafanyabiashara walio chini ya Jumuiya hiyo kuja nchini Tanzania kuwekeza katika viwanda, kilimo na shughuli nyingine za biashara na uwekezaji.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mwandishi punguza jazba na muonekano wako dhahiri dhidi ya uzalendo kwanini useme raisi kakomalia mchanga wa baharini wakati ukweli unaujua ule sio mchanga wa baharini una onyesha dharau kubwa sana juu ya juhudi za raisi za kuikomboa mali ya watanzania zilizogeuzwa shamba la bibi zilikuwa zikichotwa bila huruma kutokana na watu kama wewe wasiokuwa na uzalendo

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad