IKIWA imebaki siku moja kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti mjini Dodoma, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefunguka jinsi itakavyoibana serikali kwa kuwasilisha bajeti ‘hewa’ kwa mwaka huu wa fedha unaomalizika.
Aidha, kambi hiyo imesema itakutana na kujadili mapendekezo ya serikali kuhusu ukomo wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2017/18 ambayo imebaini kwa kiasi kikubwa hayaakisi uhalisia.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliiambia Nipashe jana kuwa wamesikitika kuona bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka huu wa fedha imetekelezwa kwa kiwango kidogo.
Hata hivyo, uongozi wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umesema wabunge wa chama hicho tawala watajadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu na kupitisha bajeti ya mwaka ujao bila kujali lawama zinazoelekezwa na upinzani kwa serikali.
Nipashe ilitaka kujua kutoka kwa Mbowe mambo ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni unakwenda kuyasimamia wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti na vipaumbele vya kambi hiyo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Mbowe alisema kambi hiyo inaendelea vikao vyake vya kujadili bajeti hizo ya mwaka huu na ujao kwa kina kabla ya kuwasilisha mapendekezo yake na kuibana serikali bungeni.
Alisema kwa sasa wanafanya uchambuzi wa bajeti inayoelekea ukingoni kujua imetekelezwa kwa kiasi gani na maeneo yepi hayajatekelezwa na serikali, sababu za kushindwa kutekelezwa kwa bajeti na funzo inatoa lake kuelekea bajeti mpya ambayo itakuwa ya pili kuidhinisha na Bunge chini ya uongozi wa Rais wa tano, John Magufuli.
“Tunasikitishwa kwamba bajeti tuliyopitisha bungeni na inayotekelezwa ni vitu tofauti sana," Mbowe alisema.
"Taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango (Dk. Philip Mpango) wiki iliyopita (Machi 28) ilionyesha dhahiri kwamba fedha za maendeleo ambazo zingesaidia kunyanyua sekta nyingi zilipatikana kidogo sana na baadhi ya sekta hazikupata fedha kutokana na uwezo mdogo wa kiserikali.
“Wakati hali ikiwa hivyo, serikali inasema imeongeza mapato na inakusanya kwa wingi wakati hali hiyo siyo kweli.
“Bajeti ya mwaka 2015/16 ilikuwa ni Sh. trilioni 23 na bajeti ya kwanza ya Rais Magufuli (2016/17) ilikuwa Sh. trilioni 29.5.
Alikuja na mipango mingi, akapandisha bajeti hadi trilioni 29, tulihoji sana wakati wa mjadala wa bajeti mwaka jana kuwa haiko sawa na serikali haina uwezo wa kuongeza mapato ya kukidhi vigezo vya bajeti.
"Matokeo yake tukajipangia mipango mingi, tukapanga shughuli za maendeleo, matokeo yake tukagundua serikali haina fedha na imekopa sana. Hii inazidi kuongeza mzigo kwa mkulima na Deni la Taifa.”
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema wakati ikijua utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu umekuwa wa kusuasua, serikali imekuja na bajeti kubwa zaidi ya Sh. trilioni 31.69 kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha.
“Tunaendelea kuwadanganya wananchi katika mambo ambayo tunajua hatutatekeleza au serikali ije na mpango wa kukopa zaidi. Kukopa siyo jambo jema la kujisifia kuwa kila siku mnakopa bila mpango,” alisema.
Mbunge huyo wa Hai mkoani Kilimanjaro, alibainisha kuwa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha bado haujafika hata asilimia 40 ya bajeti iliyotengwa hivyo haoni sababu za serikali kuja na bajeti kubwa zaidi ya Sh. trilioni 32.
“Baada ya kumaliza uchambuzi wetu, tutatoa msimamo wetu wa kibajeti na mwelekeo wa kisera wa namna gani tunafikiri ni sahihi uchumi wetu uelekezwe,” alisema Mbowe.
KIPAUMBELE CHA UPINZANI
Mbowe alisema upinzani unakwenda kwenye Bunge la Bajeti ukiwa na kipaumbele cha uchumi wa vijijini na uchumi wa kilimo.
“Hili (kilimo) ni eneo ambalo safari hii kambi ya upinzani tutalipa kipaumbele katika kila bajeti tutakazowasilisha. Tunaona eneo hili serikali ya Magufuli imelisahau kabisa, hazungumzii kilimo mahali popote bali reli, ndege mambo ya usafirishaji tu,” alisema.
Mbowe alisema kambi ya upinzani imeona kuwa kilimo kinagusa asilimia 70 ya wananchi na kitendo cha serikali kutokipa kipaumbele wanakiona ndiyo sababu kubwa ya kutopungua kwa umaskini nchini.
"Katika mwaka wa fedha uliopita kilimo kilikuwa asilimia 3.4 ya Pato la Taifa, lakini lilikuwa anguko la asilimia mbili ikionyesha kuwa kinashuka zaidi wakati kinahudumia wananchi wengi zaidi,” alibainisha.
Mbowe aliongeza: “Kama kilimo kinashindwa kuchangia kwenye Pato la Taifa, maana yake wakulima wako hoi, na kama serikali haikupeleka fedha kwa wakulima, umaskini hautaisha nchini.”
KAULI YA CCM
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza, akizungumza jana, alisema wabunge wa chama chake watajadili na kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/18.
Rweikiza alisema wabunge wa CCM wanatarajia kuona fedha zitakazopatikana zinaelekezwa kwenye miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja.
Mbunge huyo wa Bukoba Vijijini mkoani Kagera alisema: “Tungependa fedha zipatikane, ziende kutekeleza miradi ya wananchi kwenye sekta ya maji, elimu, afya na mingine. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo uwaguse moja kwa moja wananchi wa kawaida.”
Alisema miradi ya maendeleo itatekelezwa ikiwa serikali itaendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 ambao Waziri Mpango ameshakiri umekuwa wa kusuasua, Rweikiza alisema wabunge wanaijua nchi na uchumi ulivyo.
“Tunapopitisha bajeti, siyo kwamba kuna kapu fulani tutaenda kutoa na kutumia, bali tunaweka bajeti kwamba tutumie kiasi fulani kilichoidhinishwa kulingana na upatikanaji wa fedha,” Rweikiza alisema.
“Zikipatikana hiyo kazi inafanyika, kama haijafanyika tunajua ukaguzi ukifanywa na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), tutajua ilipatikana kiasi gani na ilitumika kiasi gani na kama haikupatikana, huwezi kumlaumu mtu.”
Machi 28, Dk. Mpango aliwasilisha bungeni bajeti elekezi ya Sh. trilioni 31.69 kwa mwaka ujao wa fedha huku akibainisha changamoto tano zilizokwamisha utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu.
Waziri huyo alisema serikali ilipanga kutumia Sh. trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Kati yake, Sh. trilioni 8.702 zilikuwa za ndani na Sh. trilioni 3.117 ni fedha za nje.
Hata hivyo, Dk. Mpango alibainisha kuwa hadi kufikia Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa ni Sh. trilioni 3.975 ikijumuisha fedha zilizotolewa kwa Halmashauri, sawa na asilimia 34 ya bajeti yote ya maendeleo.
“Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani zilikuwa Sh. trilioni 3.103 na fedha za nje Sh. bilioni 871.8,” Dk. Mpango alisema.
Waziri huyo alisema kutotekelezwa kwa bajeti hiyo ni pamoja na kuelekeza sehemu ya fedha kulipia madeni ya miradi ya maendeleo, na kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu.
Nyingine ni kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha kimataifa, matayarisho hafifu ya miradi na mwamko mdogo wa kulipa kodi hususan uzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).
BAJETI ‘HEWA’
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari mwaka huu, jumla ya Sh. trilioni 16.152 zilitolewa kwa wizara, idara zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, sawa na asilimia 54.68 ya bajeti yote iliyoidhinishwa na Bunge.
Kati ya hizo, Dk. Mpango alisema Sh. trilioni 12.177 (sawa na asilimia 41.22 ya bajeti yote) zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Sh. bilioni 126.3.
VIPAUMBELE VYA SERIKALI
Kwa mujibu wa Dk. Mpango maeneo ya kipaumbele kwa mwaka ujao wa fedha ni ujenzi wa reli, ukamilishaji malipo ya ununuaji ndege tatu za serikali, mradi wa chuma Liganga, makaa ya mawe Mchuchuma, uanzishwaji wa kanda maalumu za kiuchumi ambazo ni Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na Mtwara, miradi ya gesi asilia, shamba la kilimo na uzalishaji sukari Mkulazi.
Serikali pia inapanga kuendelea na miradi mingine ya kipaumbele ambayo ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa eneo la viwanda Tamco, Kiwanda cha General Tyre mkoani Arusha, mradi wa magadi Soda, kuimarisha mfumo wa taifa wa maendeleo ya wajasiriamali, na uendelezaji wa viwanda vidogo na ujenzi wa ofisi za Sido.
Mingine ni kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara, kuimarisha mitaji na kutumia benki za ndani za maendeleo TIB na TADB, na kuhamishia shughuli za Serikali Kuu makao makuu Dodoma ambapo tayari wizara zimeelekezwa kutenga fedha.
VIBANO
Katika mkutano ujao wa Bunge, serikali inatarajiwa kubanwa kutoa maelezo kuhusu kutotekelezwa kwa mpango wa kutoa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji/ mtaa. Ofisi ya Waziri Mkuu iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 59 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kutekeleza ahadi hiyo ya Rais Magufuli.
Serikali pia inatarajiwa kubanwa na Bunge kutokana na kutotoa ajira kwa wananchi na pia kutolipa malimbikizo ya madeni ya watumishi wa umma. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliahidi kutoa ajira 71,496.
Kibano kingine ni kwenye miradi ya maji, ujenzi wa meli mpya Ziwa Victoria na ukarabati wa meli zilizopo kwenye maziwa makuu, uhaba wa dawa, vifo cya uzazi na utapiamlo, ongezeko la watu nchini, ahadi ya zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata, ufufuaji wa Kiwanda cha General Tyre na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Serikali pia inatarajiwa kubanwa ili kutoa maelezo ya kina kuhusu kitendo cha wizara sita kuweka ofisi kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), utekelezaji wa ununuzi na ugawaji wa pikipiki kwa Waratibu Elimu Kata wa mikoa 18 na kuchangia mafuta kwa ajili ya magari na pikipiki hizo.
Kibano kingine kwa serikali kinatarajiwa kuwa faida ya mradi wa mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa nyumba za walimu na watumishi wengine wa umma na uzingatiaji wa sheria ya manunuzi ya umma katika ununuzi wa ndege mpya za serikali.