Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewahimiza wananchi kudumisha na kuuenzi Muungano wa Taganyika na Zanzibar na kuwahakikishia wananchi wa pande Mbili kuwa kero chache za Muungano ambazo zimebaki zitamalizwa kwa mazungumzo kama hatua ya kudumisha Muungano huo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika Mahojiano na vyombo Mbalimbali vya habari katika kuelekea katika Kilele cha Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo sherehe za kitaifa mwaka huu kwa mara ya Kwanza zitafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa tangu Muungano huo uasisiwe umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote Mbili kwani jamii zimefahamiani na kushirikiano vizuri katika shughuli za kiuchumi na za kimaendeleo hasa uimarishaji wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa pande Mbili.
Aidha,Amesema hatua zinazochukuliwa za kutatua kero za Muungano kwa haraka ni jambo jema na la msingi kwani linalenga kuhakikisha Muungano ambao umefikisha miaka 53 sasa unakuwa ni Muungano wa mfano wa kuigwa Duniani.
Kuhusu elimu ya Muungano wa Vijana, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema upo umuhimu mkubwa kwa taasisi za Kiserikali za pande Mbili kuweka mikakati mizuri ya kuelemisha vijana wa sasa kujua umuhimu wa Muungano ili waweze kuuelewa na kuudumisha.
Amesema kwa sasa vijana wengi wanafuatilia sana mitandao ya kijamii hivyo ni muhimu kwa taasisi za kiserikali zinazoshughulia Muungano kuweka utaratibu wa kupeleka ujumbe mbalimbali kuhusu Muungano kwa jamii hasa vijana kwa ajili ya kuwaelimisha faida za Muungano.
Makamu wa Rais pia amehimiza makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo viongozi wastaafu nchini waendelee na jitihada zao katika kuelimisha umma ili kuuelewa vizuri Muungano kwa ajili ya faida ya jamii nzima na ya Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
DODOMA.
25-April-2017