Walinzi wa Rauis walimpiga risasi na kumuua mtu aliyeingia kwenye ikulu ya Kenya, Jumapili ya majuzi wakati Rais Uhuru Kenyatta akihudhuria mashindano ya golf huko Muthaiga, kwa mujibu wa gazeti la Sunday Nation.
Katika tukio hilo ambalo limebaki kuwa siri kubwa wakati uchunguzi ukiendelea, mtu huyo asiyefahamika na mwenye umri wa makamo, alidaiwa kuingia bila ruhusa kwenye maeneo yanayolindwa vikali kabla ya saa 11 jioni na alikuwa kwenye eneo la maegesho, si mbali sana na jengo lenyewe na ndipo walinzi walipomuona.
Vyanzo vimeliambia gazeti hilo kuwa maafisa wa usalama wanaamini mtu huyo aliruka uzio wa ikulu hiyo sababu haiwezekani kuingia ndani bila kupita getini ambako nako hadi uruhusiwe.
Hii ni mara ya kwanza mtu yeyote kupigwa risasi na kuuawa ndani ya viwanja vya ikulu, lakini hilo ni tukio la tatu kwa mtu kuingia bila ruhusa tangu Rais Kenyatta ahamie humo mwaka 2013.
Chanzo kimoja kimesema mtu huyo alikuwa na kisu na kingine kudai hakuwa na silaha. Mwili wake ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti jijini Nairobi na hadi Ijumaa hakukuwa na mtu aliyeenda kuulizia.