MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), amemwangukia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa kumuomba amsaidie kutatua changamoto ya maji inayowakabili kwa muda mrefu wananchi wa jimboni kwake.
Ridhiwani alitoa ombi hilo juzi katika ziara ya Waziri Mkuu Majaliwa aliyoifanya jimboni humo kwa lengo la kutembelea chanzo cha maji kilichopo Mto Wami, kama sehemu ya kukagua utekelezaji wa mradi wa maji wa awamu ya tatu wa Wami-Chalinze.
“Changamoto ya upatikanaji wa maji jimboni Chalinze, bado ni kubwa na inahitaji nguvu ya ziada ili kufikia malengo ya kuhakikisha wananchi wanapata maji kama ilivyokusudiwa na Serikali.
“Suala la maji kwa Jimbo la Chalinze, imekuwa kama sehemu ya siasa na si huduma kwa kuwa tangu mradi wa awamu ya kwanza wa Wami –Chalinze uanze kutekelezwa, ni vijiji 20 tu vya mwanzo ndivyo vilivyopata maji.
“Ieleweke kwamba, Mkoa wa Pwani ni mkoa ambao unakua kwa kasi na una viwanda vingi. Hivyo basi, mahitaji ya maji ni makubwa zaidi ukilinganisha na awali.
“Kwa hiyo, kama hakutakuwa na mpango madhubuti wa kupatikana kwa maji ya uhakika, viwanda vitakufa kwa sababu huwezi kuendesha kiwanda kinachohitaji maji wakati huna maji,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa aliwahakikishia wananchi wa Jimbo la Chalinze, kwamba watapata maji ya uhakika baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa awamu tatu utakaogharimu Dola za Marekani milioni 41.362.
Alisema kwamba, Serikali imekuwa na msukumo wa kutoa huduma ya maji ya uhakika kwa wananchi wake na kwamba wananchi wawe na uvumilivu kwa kuwa Serikali inatambua shida yao ya maji.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Greyson Lwenge, kumsimamia mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo wa maji.