Kutokana na ushirikiano uliopo kati ya nchi ya Tanzania na China, lugha ya Kichina imeelezwa kuwa ni fursa ya ajira kwa Watanzania hivyo inatakiwa kufundishwa hasa katika vyuo.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Mkuu wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere(MNMA), Dk Thomas Ndaluka wakati wa warsha ya utamaduni wa China iliyofanyika kwenye chuo hicho.
“China na Tanzania ni marafiki hivyo ni muhimu kujua utamaduni wa kila mmoja, lakini Watanzania wanapojifunza Kichina wanapanua wigo wa kuweza kuajirika kwenye kampuni za China,” alisema.
Aidha, alisema lengo hilo linaenda sambamba na kuhamasisha ufundishaji wa Kiswahili kwa Wachina.
“Sisi kama Tanzania tunafanya juhudi za kufundisha Kiswahili kwa wageni kupitia kozi zetu na hata Watanzania wanaokwenda nchini China kwa masomo au kikazi wana nafasi kubwa ya kuendeleza Kiswahili,”alisema.
Mratibu wa Kozi ya Kichina wa Chuo hicho, Dk Phillip Daninga alisema uhitaji wa kujifunza lugha hiyo umeongezeka kutokana na fursa zilizopo kupitia lugha hiyo.
“Hadi sasa kuna Watanzania zaidi ya 600 wanaojifunza Kichina. Pia, takribani wahitimu 5,000 wa lugha hiyo wameajiriwa na kampuni za China hapa nchini,” alisema Dk Daninga.
Dk Daninga alisema kuwa chuo hicho kipo mbioni kuanzisha kozi ya Kichina kwa ngazi ya diploma na shahada mara baada ya kupata kibali cha Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (Nacte).
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuendeleza Kichina iliyopo ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Liu Yan alisema kuwa Taifa hilo linatambua uhusiano uliopo na umuhimu wa kujua utamaduni kuwa ni suala la msingi.
“Ni muhimu kutambuana kila mmoja, walimu kutoka China wanajifunza Kiswahili na sisi tunahamasisha Watanzania wajue Kichina,”alisema Profesa huyo.