Kupoteza askari wetu nane katika tukio la mauaji huko Kibiti Pwani kunapaswa kumshtua kila Mtanzania. Binafsi ninatoa pole za dhati kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu wote. Ni matumaini yangu uchunguzi wa kina utafanyika ili kubaini wahusika wa tukio hili na kujairbu kwa namna yote inayowezekana kuzuia kutokujirudia tena.
Kwa tunaotoka familia za polisi siku hii ni nzito na ya majonzi sana na inafikirisha.Wazazi wangu wote wawili walilitumikia jeshi hilo mmoja hadi mauti mwingine hadi kustaafu. Kaka na dada zangu wanalitumikia na sasa wengine wamebakisha miaka michache kustaafu na sasa binti yangu mmoja tayari analitumikia jeshi hili. Hivyo, habari hii ni habari inayogusa fikra na hisia. Fikra kwa sababu ni tukio ambalo hata bila kuwa na undugu na yeyote linashtusha, linaumiza, na lisababisha maswali mengi ambayo majibu yake si rahisi kuyakisia. Ni la hisia kwa vile linahusu maisha ya binadamu wenzetu ambao wameondolewa na binadamu wengine na hasa wakiwa katika kazini.
Fikiria tu kuwa wangapi humu kazi zao zinahusisha uwezekano wa kutokurudi nyumbani kila siku kwa kushambuliwa na watu wengine? Polisi kila anapoamka kutoka inaweza ikawa ni siku yake ya mwisho kwani anaweza kuuawa. Wengi tunaamka na inaweza ikawa siku ya mwisho lakini hofu ya kuuwa siyo hofu ya msingi inayotembea nasi kila siku.
Hawa ni mashujaa wetu, ni mashujaa ambao tunatakiwa tuwatambue na kuwaenzi hivyo. POlisi kama vile wanajeshi ndio watumishi pekee wa umma ambao wanaitwa hadi kuyatoa maisha yao ili kulilinda taifa. Kama Taifa pamoja na tofauti zetu zote ni lazima tuwatambue kama hivyo na kuonesha shukrani.
Ni matumaini na maombi yangu kwa Watanzania wote ambao wataweza mahali pote kujitokeza kwa wingi siku ya kuwaaga mashujaa hawa ili kutuma ujumbe usio na utata kuwa pamoja na matatizo yetu yote, pamoja na changamoto zetu zote kama taifa tunasimama na polisi wetu na tunawashukuru kwa kujitoa kwao na kuwa hatutaacha mtu au kikundi cha watu kufanya matukio kama haya.Mtuwakilishe hata sisi tulio mbali au wale ambao wangependa kuwepo katika makundi ya kuwaaga mashujaa hawa wa taifa letu.
Tujifunze kutoka nchi kama Marekani ambapo pamoja na changamoto zote walizo nazo kuhusiana na polisi wao lakini polisi wakiuawa wakiwa kazini ni pigo linalogusa nchi nzima. Kwani, nchi ya kidemokrasia inasimama au kuanguka na polisi wake.
Ni maombi yangu sasa Jeshi la Polisi (Wizara ya Mambo ya Ndani) ianze makaburi maalum ambapo mashujaa hawa watastahili kulazwa na kukumbukwa na vizazi vingi vijavyo. Yatakuwa ni makaburi ya mashujaa wetu ambao wanapoteza maisha yao wakiwa kazini. Tunaweza kuyaita "National Heroes Cemetery" - Makaburi ya Mashujaa wa Taifa. Na inaweza kufikiriwa nani wengine watastahili kulazwa kwenye makaburi hayo lakini askari wanauawa kazini watalazwa hapo.
Mungu azilaze pema roho za mashujaa wetu marehemu!
Saluti!