Upo uwezekano mkubwa wa wewe kuongeza uwezo wako wa kupata pesa zaidi ya hapo ulipo ikiwa utafuata misingi sahihi ya pesa jinsi inavyotaka. Kila kitu kina kanuni zake ikiwamo hata kanuni za kupata pesa.
Kama bado unashangaa kwa nini wengine wana pesa nyingi na wewe huna, hiyo yote ni kwa sababu wanazifanyia kazi kanuni za pesa bila kujali wanazitumia kwa bahati mbaya au kwa kujua.
Huna haja ya kuendelea kukosa pesa kila wakati. Umefika wakati wa kukubali kujifunza na kutumia kanuni za pesa ili zikusaidie kuongeza uwezo wako wa kupata pesa na kufanikiwa maishani mwako.
Kupitia makala haya, naomba nikuachie dondoo kadhaa zitakazoweza kukusaidia moja kwa moja kuongeza uwezo wako wa kupata pesa na kuwa mtu wa mafanikio. Karibu tujifunze kwa pamoja;-
1. Jifunze mambo ya pesa kila siku.
Jifunze kwenye vitabu, pia jifunze kwenye semina. Huwezi kufanikiwa kipesa kama hujachukua hatua za kujifunza jinsi pesa inavyofanya kazi.
Unalazimika kujua jinsi pesa inavyoweza ikawekezwa na kudumu katika maisha yako. Yote haya hayawezi kuja kwenye upande wako kama uchawi bali ni kwa wewe kuweza kujifunza.
2. Tafuta mshauri (Mentors) atakayekuwa anakuongoza kwenye mambo yako ya pesa pale unapokwama au unataka kusonga mbele zaidi. Hili linaweza kuwa jambo ni dogo kwako lakini ni muhimu kwako.
Watu karibu wote ambao wana mafanikio kila siku wana watu ambao wanawafuata au wanawashauri kila mara katika mambo ya pesa. Hali hiyo hupelekea kuwaweka juu kimafanikio.
3. Kama upo kwenye madeni, tafuta namna ya kuondoka huko. Madeni ni sumu kubwa ya mafanikio kama utakuwa nayo kwa muda mrefu. Kama una madeni mengi, upo uwezekano wa nidhamu yako ya kipesa ikawa mbovu.
Weka mpango imara ambayo itaweza kukutoa kwenye madeni na kuanza kuishi kwa uhuru wa kifedha. Hutaweza kufika mbali kimafanikio ikiwa kila wakati ni mtu wa kudaiwa, hutaweza kufanya kitu chochote.
4. Jilipe wewe kwanza kila ukipata pesa yoyote ile. Kila aina ya pesa unayoipata, tenga kiasi kidogo na ujilipe kama mtafutaji wake. Usiache kujilipa hata kama pesa uliyopata ni kidogo.
Pesa ile ambayo utakuwa unajilipa wewe kwanza, huna haja ya kuwa nayo na haraka kuitumia. Kama ambavyo tumekuwa tukisema iache iwe nyingi baada ya hapo iwekeze.
5. Tafuta namna pesa zako zitakavyoweza kukulinda pale unapokuwa umeumia au kufa na kuacha watoto wadogo. Kuwa na ulinzi wako kama bima vile, lakini wewe bima yako inaweza ikawa pia vitega uchumi vyako mbalimbali.
Hapa unatakiwa ujifunze kuwekeza mapema wakati bado ukijana mwenye nguvu. Kwa kadri jinsi unavyozidi kuwekeza pesa zako zitakulinda hata pale utakopokuwa umeshazeeka au kupatwa na matatizo yoyote.
Hivyo ndivyo unavyoweza kuongeza uwezo wako wa kupata pesa kama utazingatia mambo hayo matano kama yalivyowekwa wazi kupitia makala haya. Naamini umejifunza kitu na chukua hatua.