Watu hao walikuwa wamepakiana kwenye pikipiki moja huku wakiwa wamevaa hijabu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani Pwani ,Onesmo Lyanga alisema pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.
Akielezea juu ya tukio hilo alifafanua,lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya mchana ,Muhoro ,Rufiji barabara kuu ya Dar es Salaam Lindi.
“Siku ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu kila moja “
“Miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.
Alisema askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.
“Baada ya hapo walifika kizuizi cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha Muhoro “
“Hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari waliwafuatilia na wakavuka daraja la Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.
Aidha alibainisha baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.
“Majeruhi hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi”
“Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.
Lyanga alisema walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia .
Hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.