Rais Magufuli Aipa Majukumu Mazito Kamati ya Pili ya Kuchunguza Madini Katika Mchanga Unaopelekwa Nje ya Nchi..!!!


Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,  jana tarehe 11 Aprili, 2017 amewaapisha wajumbe wa Kamati Maalum ya pili ya wachumi na wanasheria itakayochunguza mchanga wenye madini ulio katika makontena yaliyopo maeneo mbalimbali nchini.

Walioapishwa ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Nehemiah Eliachim Osoro na wajumbe wake ambao ni Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara, Dkt. Oswald Joseph Mashindano, Bw. Casmir Sumba Kyuki, Bw. Andrew Wilson Massawe, Bw. Gabriel Pascal Malata, Bw. Usaje Bernard Usubisye na Bi. Butamo Kasuka Philip.

Akizungumza baada ya kuwaapisha wajumbe wa kamati hii, Mhe. Rais Magufuli alisema ameunda kamati hiyo ili ifanye uchunguzi wa kina utakaobaini aina ya madini yaliyo ndani ya mchanga huo, thamani yake, kiwango cha kila aina ya madini, uzito wa mchanga unaowekwa ndani ya makontena na pia kujua ni makontena mangapi yamepitishwa tangu mwaka 1998.

“Kafuatilieni makontena mangapi yametoka hapa nchini na kupelekwa nje ya nchi tangu mwaka 1998, na kama hayo makontena yana madini aina ya dhahabu, shaba na silva mkafuatilie tujue zimepelekwa tani ngapi za dhahabu, tani ngapi za shaba na tani ngapi za silva, je makontena mangapi yanapita kila mwezi? Makontena 1,000 au mangapi? na je zilikuwa na thamani ya kiasi gani? Je tumelipwa kiasi gani cha fedha?

“Na nyie wanasheria mfanye uchunguzi juu ya kinachofanyika na muone sheria zinasema? Tujue utekelezaji wa sheria kama unafanyika inavyotakiwa? Tunataka hoja hizi zipate majibu” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli alisisitiza kuwa wakati umefika kwa Tanzania kunufaika na rasilimali zake na kwamba Serikali haiwezi kukubali madini yaendelee kuondoka bila kuleta manufaa kwa wananchi.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. ongeeni sasa msiomtakia mema mh.magu..BIG UP MAGU.May GOD Blessing you..

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad