AMEJIRUDI. Ndivyo kitendo cha Rais John Magufuli kumteua Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kinavyoweza kutafsiriwa.
Profesa Kitila aliteuliwa jana kuchukua nafasi ya Mbogo Futakamba anayestaafu.
Tafsiri kwamba Rais Magufuli amejirudi inaweza kutumika kwenye tukio hilo kwa kurejea kauli aliyopata kuitoa akiwa Zanzibar kwenye ziara ya kushukuru wananchi wa kisiwa hicho baada ya Uchaguzi Mkuu, aliposema hakuna mpinzani atakanyaga ukuu katika Serikali yake.
Rais Magufuli alisema anamshangaa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwamba pamoja na kushinda uchaguzi kwa asilimia 92, ameweka wapinzani kwenye Serikali yake, lakini yeye hawezi kufanya hivyo.
“Kusema ukweli anayoyafanya Rais Shein yanaonesha ana moyo wa ajabu sana, mimi siwezi kuruhusu mpinzani akanyage katika Serikali yangu,” alisema.
Lakini jana, taarifa kutoka Ikulu ilibainisha kuwa Rais Magufuli amemteua Profesa Mkumbo kushika wadhifa huo akitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Profesa Mkumbo anakuwa mpinzani wa pili kupewa wadhifa ndani ya Serikali ya Magufuli, wa kwanza akiwa Dk Augustino Mrema aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Parole. Mrema ni Mwenyekiti wa TLP.
Katika uteuzi wa jana wengine walioteuliwa ni Dk Leonard Akwilapo ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo.