SIASA za Ukanda wa Afrika Mashariki zimechukua sura mpya baada ya Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa kutangaza rasmi kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.
Kenyatta aliyeunga ushirika pamoja na William Rutto, anaingia katika kinyang’anyiro cha kuwania awamu ya pili ya kuiongoza Kenya huku upande wa upinzani ukiwa umepitisha jina la Raila Odinga kupeperusha bendera ya upinzani.
Wakati Lowassa akitangaza kumuunga mkono Kenyatta, kwa upande wake Odinga tayari ilishajulikana wazi urafiki wake na Rais Dk. John Magufuli ambao umeanza miaka mingi tangu akiwa Waziri wa Ujenzi.
Hatua hiyo ya Lowassa ambaye anatajwa kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi nchini na Afrika Mashariki imekuja baada ya kutembelewa jana nyumbani kwake Monduli na wabunge zaidi ya 20 na maofisa kutoka Kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
"Mimi naamini Uhuru Kenyatta anao uwezo mkubwa wa kuwaunganisha vema wananchi wa Kenya na Watanzania. Naahidi ukifika muda muafaka tutaungana naye kumsaidia katika kampeni zake, alisema Lowassa na kuongeza:
“Pamoja na kumtumikia Mungu lakini pia kwa moyo wa dhati, mimi na wananchi wa Monduli tunamuunga mkono Kenyatta katika mbio za uchaguzi nchini Kenya".
Alisema ushawishi wake kwa Kenyatta umejengwa na imani kubwa aliyonayo kwa Rais huyo akiamini kwa dhati kwamba ana uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hasa Tanzania na Kenya.
"Natamka wazi na dunia yote ijue kuanzia sasa kwamba sisi tunampenda Uhuru Kenyatta na yeye anajua kama tunampenda, kwa hiyo tunamuunga mkono tukiamini kabisa ana uwezo wa kuunganisha wananchi wetu,” alisema Lowassa.
Katika tamko lake, Lowassa mwanasiasa mwenye ushawishi nchini Kenya pia kupitia jamii ya Kimaasai aliwasihi wananchi wa Kenya kutokufanya makosa katika uchaguzi ujao.
“Niwaombe wananchi wa Kenya kuhakikisha Rais Kenyatta anarejea madarakani tena kwenye uchaguzi ujao,” alisema Lowassa.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo mzito uliofika nyumbani kwake na kushiriki pamoja chakula, Naibu Spika wa Kaunti ya Kajiado Dk.Lanoi Parmuat alimtaka Lowassa katika siasa zake ahakikishe anawashika mkono zaidi wanawake.
Alisema kina mama katika jamii ndiyo wenye moyo na msimamo thabiti wa kuhakikisha wanamfikisha kwenye ndoto zake za siasa.
“Kwa sasa tunaendesha harakati za kuhakikisha kina mama wa ukanda huu wa Afrika Mashariki wanakombolewa katika elimu,” alisema Lanoi na kuongeza:
“Na kwa kupitia hatua hiyo tayari tumewatembelea marais wa Uganda, Ethiopia na Rwanda na leo tumefika kwako ujumbe wetu mkubwa ukiwa ni ukombozi wa elimu kwa mtoto wa kike.
“Pamoja na ujumbe huu kufika kwako kukusalimia tunapenda pia kukuhakikishia kwamba tunaendelea kukuombea kwa Mungu katika uchaguzi ujao wa Tanzania 2020 uweze kuibuka na ushindi hayo ni maombi yetu kwa Mungu”.
Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga aliushukuru ujumbe huo kwa kuonyesha upendo kwa wanananchi wa Monduli na Watanzania kwa heshima waliyoionyesha ya kumtembelea Lowassa nyumbani kwake na kumtia moyo.
Uchaguzi wa Kenya unatarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu huku kukiwa na mchuano mkali kutoka kwa wagombea urais kutoka vyama mbalimbali.