ACHANA na stori za vichochoroni. Straika wa Uganda, Emmanuel Okwi ameitumia Mwanaspoti kuwaambia mashabiki wa Simba kwamba wakae mkao wa kula msimu ujao huku akitoa ujumbe spesho kwa wachezaji wa Msimbazi.
Simba wamemdaka Okwi juu kwa juu lakini kwavile muda ulikuwa mdogo, alipotoka Sweden akaamua kujiunga na SC Villa kujifua zaidi na kufuta maneno ya watu waliokuwa wakidai kwamba amefulia kinoma.
Mwanaspoti imefanya mahojiano maalumu na Okwi jijini Kampala na kuweka wazi kwamba Simba ni kama nyumbani kwake na muda wowote atatua kuwatendea haki wala wasiwe na mchecheto.
“Simba ni kama nyumbani, nitarudi Simba, hata wakati wa dirisha dogo ningekuwa nimerudi tulizungumza na kila kitu kilikwenda vizuri, kilichokwamisha ni uhamisho maana dirisha lilikuwa limefungwa na sheria hazikuruhusu. Nafurahia maisha ya Simba, wananipenda si viongozi wala mashabiki hata mimi nawapenda na ninapaswa kuonyesha ushirikiano juu yao.
“Sasa hivi mimi nipo, milango yote ipo wazi ndiyo maana nimesema Simba narudi muda wowote kwani wamenifurahisha katika maisha yangu, ingawa miezi iliyobaki kwa ajili ya msimu mpya wa ligi huwezi kuzungumza zaidi maana lolote linaweza kutokea kwangu ama kwa viongozi wa Simba japokuwa kila kitu kinakwenda vizuri,” alisema Okwi akizungumza na Mwanaspoti ambalo ndiyo gazeti pekee la Kiswahili Afrika Mashariki linalochapishwa Kenya na Tanzania.
“Ukiachana na mambo ya uhamisho lakini wengi walijua kiwango changu kimeshuka sikucheza kwa muda mrefu, yaani nilipoteza uaminifu kwa watu, ni jambo ambalo liliniumiza sana, kipindi hiki nimeiva kisoka na nimerudi kwenye ubora wangu mimi ni yule Okwi wa mwanzo,”alisisitiza mchezaji huyo.
Okwi anaombea kila dakika Simba ifanikiwe kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu; “Natamani na kila siku huwa naiombea Simba watwae ubingwa na washiriki michuano ya Kimataifa, wanashika nafasi ya kwanza ingawa hawana tofauti kubwa ya pointi na wapinzani wao Yanga, hivyo wakati huu kwa wachezaji wa Simba ni wakati wa kupambana na kuonyesha ni jinsi gani wanaume wanatakiwa kuleta maendeleo ya klabu. Hapo wajitoe sana.
“Naamini uwezo wanao kwani kikosi chao ni kizuri na nimekuwa nawafuatilia kila hatua kwa hakika ubingwa ukienda Simba nitafurahi sana. Mipango yangu ikienda kama ilivyokuwa basi nikirejea Simba msimu ujao itakuwa ni timu tishio kwani hata sasa kuna vijana nawafuatilia kwa karibu wanaonyesha kupambana.
“Yanga wala hawanitishi, ni timu ya kawaida ingawa hupaswi kuwadharau kutokana na kiwango chao kwa sasa, ndiyo maana nasema wachezaji wa Simba wanapaswa kujitoa kwa kila hali ili watwae ubingwa,” alisema Okwi.