Rasmi..Wahusika wa Wizi wa Mabilioni ya Tegeta Escrow Kukiona cha Moto..!!!


UCHUNGUZI mpya kuhusu kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti Maalumu ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umekamilika.

Uchunguzi huo umefanywa na jopo la wataalamu wanne waliobobea katika masuala ya fedha kimataifa.  

Timu ya uchunguzi huo inaongozwa na Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Donald Kaberuka ambapo wajumbe wengine ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Benki ya Dunia (WB), James Adams, Steve Kayizzi Mugerwa ambaye aliwahi kufanya kazi AfDB na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pamoja na Mugisha Kamugisha.

Timu hiyo ilianza kufanya uchunguzi huo Aprili mwaka jana na wakati wowote kuanzia sasa itakabidhi ripoti yake serikalini.

Hatua hiyo ya kukamilika na kukabidhiwa kwa ripoti hiyo Serikalini huenda wahusika wakaonja joto ya jiwe kwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alisema waliamua kufanya uchunguzi huo ili kurejesha mahusiano yao na wahisani.

Katibu huyo alikuwa akizungumza baada ya kusaini makubaliano baina ya Serikali na Umoja wa Ulaya (EU) ambao umeahidi kutoa Euro 205 (sawa na Sh bilioni 490) kusaidia bajeti ya serikali.

“Utafiti huu unaongozwa na Dk. Donald Kaberuka na unaangalia historia nzima ya yale yote yaliyotokea wakati wa Tegeta Escrow ili matatizo yasije kujirudia tena.

“Escrow imetupa fundisho, tumepata uzoefu na sasa tumerudi kwenye ‘dialoge’, tunajaribu kufanya utafiti ili kuwarudisha wahisani wa maendeleo wawe na moyo ule ule.

“Tumekaa nao mezani na kati ya mambo ambayo tumekubaliana pale itakapotokea kuna matatizo kama ya Tegeta Escrow hatutaki yazuie utekelezaji wa mipango mingine. Kwenye mkataba huu tatizo hilo halitatokea tena.

Mmoja wa wajumbe wa timu hiyo, Kamugisha, alisema sehemu ya mapendekezo ya ripoti ya tume hiyo tayari yameanza kufanyiwa kazi.

“Agosti mwaka jana tuliwapa mapendekezo wakayaangalia, mwezi uliopita tulikuwa na semina ya kumalizia Dodoma na juzi tulipata feedback (mrejesho) na sasa tunakamilisha taarifa ya mapendekezo ya namna ya kushughulika ili tusitumbukie tena katika mtaro.

“Sehemu ya hatua ambazo tayari zimeanza kuonekana ni mojawapo ya mapendekezo yetu, mfano mfumo wa mashauriano kati ya EU na serikali na EU wamechukua vitu vizuri vilivyo kule (ripoti) na wanaanza kuvifanyia kazi,” alisema Kamugisha.

Alisema walipewa kazi ya kutafuta kiini cha chimbuko la kashfa hiyo na kupendekeza nini kifanyike ili kuepuka kurudia makosa.

“Baada ya mtafaruku wa Escrow ilionekana kwamba tulivyolishughulikia haikuwa sawasawa, na kama watu mnashirikiana hamuwezi kusema hamtatofautiana, hivyo walisema tutafute utaratibu mzuri ili likitokea jambo kama hili tusipate matokeo mabaya tena.

“Tulipewa kazi ya kutafuta ni kwanini mambo yalikwenda kama yalivyokuwa mwaka 2014 na nini kifanyike ili pande hizi mbili (serikali na wahisani) ziweze kuzungumza na kuelewana,” alisema.

CHIMBUKO LA KASHFA YA ESCROW

Escrow ni akaunti iliyofunguliwa ilipotokea wabia wawili walipokuwa na ugomvi kuhusiana na mapato yao.

Kampuni ya VIP Engineering inayomilikiwa na James Rugemalila na Kampuni ya Mechmar walikuwa wabia walioanzisha biashara pamoja kupitia kampuni ya IPTL. Mradi huu harufu yake ilianza mwaka 1994, ukawa na mgogoro mkubwa, ukachelewa kuanza rasmi hadi mwaka 2000.

Mwaka 2006 waliingia mgogoro, hivyo ikabidi wapelekane mahakamani na kadiri siku zilivyokwenda wakalazimika kufungua akaunti ya kuhifadhi fedha zilizotoka Tanesco kutokana na kuzalisha umeme zijulikanazo kama ‘capacity charge’. 

Uchunguzi wa kuchotwa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow na kuuzwa mitambo ya kufua umeme ya IPTL kwa Kampuni ya Pan Africa Power (Tanzania) Limited (PAP), umefikisha miaka miwili sasa.

Jalada la usajili wa Kampuni ya PAP mpaka sasa linaendelea kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi.

Kutokana na kashfa hiyo baadhi ya nchi wahisani zilitangaza kuikatia misaada serikali ya zaidi ya Sh trilioni 1.

Hatua hiyo ilisababisha Bunge la 10 kuunda kamati ya uchunguzi wa sakata hilo ambapo ilitoa maazimio manane ikiwemo kuchukuliwa hatua kwa watu wote waliohusika katika uchotwaji huo wa fedha.

MSAADA WA BIL. 490

Msaada huo wa Sh bilioni 490 utatolewa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo kila mwaka zitatolewa Sh bilioni 120.

Akiuzungumza wakati wa kusaini makubaliano ya msaada huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Doto James, alisema EU wamevutiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika maeneo mbalimbali kama vile kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Alisema msaada huo utasaidia katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa, sekta za kilimo na maendeleo ya viwanda.  

“Huu si mkopo ni msaada usiokuwa na masharti yoyote kwenye bajeti yetu ya kila mwaka, wamevutiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano, tumeupitia na kuona ni msaada sahihi na una tija kwa taifa,” alisema James.

Alisema kabla ya kupokea msaada huo ulipitia katika taratibu za kiserikali na ukaridhiwa na kamati zilizoko kisheria kama Kamati ya Kitaifa ya Madeni.

Alisema msaada huo hauna masharti lakini wahisani wameelekeza fedha zipelekwe katika maeneo yaliyolengwa.

“Msaada huu hauna masharti ni namna tu ya maelewano, wanataka waone fedha zinapelekwa kwenye sekta za kilimo, afya, elimu na nyingine…sasa kama mtu anakusaidia ‘kuku guide’ peleka kwenye maeneo hayo si masharti ni vitu vya kawaida,” alisema.

Kwa upande wake Balozi wa EU nchini, Roeland Van de Geer, alisema wameliangalia zaidi suala la utawala kama eneo kuu katika mpango wa ushirikiano na Tanzania na vilevile wanatazamia maendeleo zaidi katika maeneo ya kilimo,ujenzi wa barabara za vijijini na nishati.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad