Ripoti ya Shirika la Amnesty International imebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokiuka haki za binadamu kwa kiasi kikubwa kutokana na dosari za kiutawala, ikiwamo kuzuia uhuru wa kujieleza, mikutano ya kisiasa na ukandamizwaji wa vyombo vya habari.
Ripoti hiyo ya mwaka 2016/17, imetoa tathmini juu ya hali ya haki za binadamu duniani ikihusisha mataifa yote makubwa na madogo na kueleza mambo kadhaa yaliyojitokeza kinyume cha misingi ya demokrasia na utawala bora.
“2016 ulikuwa ni mwaka uliotawaliwa na tabu na hofu miongoni mwa watu baada ya Serikali na makundi yaliyojihami kwa silaha (armed groups) kukiuka haki za binadamu kwa namna nyingi,” inaeleza ripoti hiyo iliyotolewa na katibu mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty.
Dosari hizo zimeonekana katika nchi mbalimbali duniani ikiwamo Afrika Kusini, Kenya, Rwanda, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na mataifa makubwa ikiwamo Marekani iliyoshutumiwa kwa ubaguzi.
Kwa upande wa Tanzania, ripoti hiyo ilizungumzia juu ya machafuko yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Zanzibar ambapo vurugu zilisababisha majeraha kwa watu 200, huku 12 wakinyanyaswa kijinsia na mmoja kubakwa.
Kasoro nyingine zilizotajwa katika ripoti hiyo ni vyombo vya usalama ikiwamo polisi kutumia nguvu dhidi ya vyama vya upinzani katika kuzuia maandamano na mikutano.
Shirika hilo limeripoti juu ya kile kilichotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar 2015 na kuelezwa kuwa CUF ilipinga uhalali wa matokeo baada ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein kushinda na wanachama zaidi ya 100 walikamatwa na vyombo vya dola.
Hata hivyo, baada ya uchaguzi huo malalamiko hayo yalipingwa kwa madai kuwa hakukuwa na kasoro na hakuna mashtaka yaliyofikishwa juu ya Jeshi la Polisi.
Kuzuiwa kwa mikutano.
Pia, ripoti hiyo imeeleza kuwa Rais John Magufuli alipiga marufuku mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020 na upinzani ulianzisha kampeni ya kupinga agizo hilo, suala lililosababisha polisi kuongeza nguvu zaidi hadi kuzuia mikutano ya ndani iliyofanywa na vyama vya siasa.
“Viongozi wawili wa upinzani pamoja na wafuasi 35 kutoka Bara na Visiwani walikamatwa na kuhojiwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo kupinga uchaguzi huo,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Uhuru wa habari
Kuhusu uhuru wa habari, ripoti hiyo imeelezea juu ya kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari, huku baadhi ya waandishi wakituhumiwa kwa madai ya uchochezi kwa mujibu wa Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Ripoti hiyo imevitaja vyombo hivyo kuwa ni gazeti la Mawio ambalo lilifungiwa pamoja na waandishi wake kushtakiwa kwa madai ya uchochezi baada ya kuripoti juu ya uchaguzi wa Zanzibar.
Pia, gazeti la Mseto lilifungiwa kwa miaka mitatu kwa kuchapisha makala juu ya rushwa huku Redio Magic na Radio Five zikifungiwa kwa muda.
Ripoti hiyo imesema wanawake wawili na wanaume sita walishtakiwa chini ya Sheria ya Mtandao kwa kutuma taarifa mitandaoni zilizohusu uchaguzi na zingine kumhusu Rais kupitia mtandao wa Facebook.
Haki za wanawake.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa Tanzania imeshindwa kutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) kumaliza ubaguzi dhidi ya wanawake ikiwamo haki ya kurithi mali.
Imegusia Sheria ya Ndoa katika kifungu namba 13 na 17 vinavyoruhusu mwanamke chini ya miaka 18 kuolewa kinyume na haki za binadamu na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni.
Wadau wanasemaje?
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kuwa taarifa hiyo ni sahihi kufuatia hali iliyokuwapo mwaka uliopita, hususan kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na kupingwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema kuwa kinachotakiwa ni wananchi wenyewe kutambua mamlaka waliyonayo dhidi ya watawala wao na kupaza sauti pale kunapokuwa na ukiukwaji wa haki au sheria.
Pia, aliwataka washauri mbalimbali wa viongozi wa juu serikalini akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutumia nafasi zao kuwasihi kufuata misingi ya sheria katika kuongoza Taifa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema ripoti hiyo inapaswa kutumika kusahihisha mahali ambapo pameleta dosari na kuzingatia misingi ya demokrasia katika utawala.
“Rais aangalie upya uamuzi wake, pengine alitaka kunyoosha pale ambapo hapakuwa sawa, lakini ameshakaa zaidi ya mwaka mmoja na sasa tunaweza kurudi katika demokrasia, “ alisema.
shughulika na vyeti feki vya paul amkonda halafu ongea mengine ni aibu
ReplyDelete