MIGODI nchini ikiwamo mikubwa ya madini ya dhahabu haijalipa kodi kwa takriban miaka 19 sasa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kupata hasara kila mwaka.
Kwa sababu hiyo, Serikali kupitia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, inaelekea kushtuka baada ya kuainisha chanzo cha kuwapo kwa hali hiyo inayoikosesha mapato.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, CAG Assad alisema tangu mwaka 1998 (miaka 19 iliyopita), hakuna mgodi unaolipa kodi kutokana na hesabu zao kuonyesha kuwa hupata hasara kila mwaka, jambo alilodai kuwa linashangaza.
"Inashangaza, wanasema wanapata hasara lakini hawaondoki. Inakuwaje wanapata hasara toka mwaka 1998 tulipoanza kuchimba madini nchini lakini hadi leo wapo tu na hawalipi kodi?" alihoji Prof. Assad.
Aidha, CAG Assad alifichua upotevu mkubwa wa mapato ya serikali utokanao na usimamizi dhaifu kwenye sekta hiyo.
Prof. Assad alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana baada ya kuwasilisha bungeni ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2015/16.
Alisema mapitio ya taarifa za fedha na taarifa za malipo ya kodi za migodi ya dhahabu ya kampuni za madini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2012 hadi 2016 yamemshangaza kwa kuonyesha kuwa migodi imekuwa ikipata hasara mfululizo.
Akieleza chanzo cha hasara hiyo, CAG alisema kwa kiasi kikubwa husababishwa na kuruhusiwa kwa kampuni za migodi kupunguza kiasi chote cha gharama zitokanazo na manunuzi ya bidhaa za mtaji (capital expenditure) kutoka kwenye mapato ya uzalishaji kwa mwaka husika.
“Mikataba mingi ya madini inaruhusu kupunguza gharama za manunuzi ya bidhaa za mtaji kwa asilimia 80 hadi 100 katika mwaka ambao bidhaa imenunuliwa kuanzia hatua za utafiti mpaka uzalishaji," alisema.
Alisema hatua hiyo husababisha kuwapo hasara mfululizo huku akibainisha jinsi kampuni kubwa za madini nchini zilivyopata hasara mfululizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2015.
Aliishauri serikali kuhakikisha inajadiliana na kampuni za madini zinazopata hasara mfululizo ili serikali itoze kodi kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mapato ghafi kulingana na Sheria ya Kodi na Mapato ya Mwaka 2004 na pia kuhakiki gharama za uwekezaji na marejesho ya kodi ili kuzuia matumizi ya mabaya ya misamaha ya kodi inayotolewa.
Alisema mikataba ya uchimbaji madini kati ya serikali na kampuni za uchimbaji katika migodi mingi ya dhahabu ilisainiwa kabla Sheria ya Kodi na Mapato ya Mwaka 2004 haijatungwa.
CAG Assad alisema viwango vya tozo za kodi kwenye mikataba hiyo vilitokana na Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 1973 na havijabadilishwa kuendana na sheria mpya ya mwaka 2004 kutokana na kuwapo kwa kifungu kinachozuia mabadiliko ya viwango vya tozo za kodi kwenye mikataba hiyo.
"Mikataba hiyo inaainisha viwango vya zuio la kodi katika ada ya usimamizi pamoja na huduma za kiufundi kati ya asilimia tatu hadi tano. Hii ni tofauti na asilimia 15 kama ilivyoanishwa kwenye Sheria ya Kodi na Mapato ya Mwaka 2004.
CAG aliishauri serikali kujadiliana na kampuni za madini kupitia kifungu kinachoruhusu kurejewa kwa mikataba kinachopatikana kwenye mikataba takribani yote ili kurekebisha viwango vya tozo za kodi kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi vinavyobadilika kufuatana na muda tangu kusainiwa kwa mikataba hiyo.
TOZO USAFIRISHAJI MADINI UGHAIBUNI
Prof. Assad alisema mapitio yake ya malipo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka kwenye migodi mikubwa minne ya dhahabu na mmoja wa almasi kwa kipindi cha kati ya mwaka 2012 hadi 2016, yalibaini kulikuwa na marejesho makubwa ya kodi hiyo kwa kiasi cha Sh. trilioni 1.144.
Alisema marejeo hayo makubwa yametokana na mianya inayotolewa na kifungu 55(1) cha Sheria ya VAT ya Mwaka 2014, sawia na sheria ya zamani, zote kwa pamoja ziliruhusu na bado zinaruhusu tozo ya kodi ya VAT kwa kiwango cha sifuri kwa bidhaa zinazosafirishwa kuuzwa nje ya nchi.
Alisema lengo la serikali kutoza kodi ya VAT kwa kiwango cha sifuri kwenye bidhaa zote zinazosafirishwa kuuzwa nje ya nchi lilikuwa ni kukuza viwanda vya ndani, lakini upungufu uliojitokeza ni kuwa sheria hiyo haikuweka makundi kuonyesha bidhaa zipi zinazostahili motisha hiyo.
"Hivyo basi, madini ambayo kwa namna yoyote lazima yauzwe nje ya nchi, nayo pia yananufaika na motisha hiyo kama vile ambavyo bidhaa za kilimo na viwandani zinavyonufaika," alisema.
Aliishauri serikali kupitia Stamico kuhakikisha bei ya ununuzi ya migodi inayokubaliwa kwenye mikataba ya ushirikiano wa kibiashara sharti itokane na upembuzi wa kina, uthaminishaji wa mali au makadirio ya madini yaliyopo nchini.
Pia aliishauri serikali kupitia upya Sheria ya Kodi ya VAT ya Mwaka 2014 na kufanya marekebisho ili kuondoa tozo za kiwango cha sifuri kwenye mauzo ya madini na vito nje ya nchi na kujadaliana na kampuni za uchimbaji madini kuhusu matokeo ya mabadiliko hayo kwenye mikataba yao (MDAs).
UTATA MAUZO YA TANZANITE
CAG alisema kuwa katika ukaguzi wake, amebaini Kampuni ya Sky Associates ilinunua hisa za umiliki wa Kampuni ya TML inayoendesha Mgodi wa Tanzanite toka kwa Kampuni ya Richland Resources Januari 30, 2015.
Hata hivyo, alisema ukaguzi wake umebaini Kampuni ya TML imekuwa ikiuzia madini ya Tanzanite kwa kampuni tanzu ya Sky Associates bila kumshirikisha mbia mwenzake ambaye ni Stamico.
"Pia, nimebaini kuwa TML inatafuta masoko na kuuza Tanzanite bila kupata ukubali wa mshirika wake Stamico ambayo ni kinyume cha kifungu cha 15.1(d-d) cha makubaliano ya ubia kati ya Stamico na TML," alisema.
Kutokana na changamoto hiyo, Prof. Assad aliishauri Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Stamico, ihakikishe mauzo ya Tanzanite yanafanyika kwa uwazi mkubwa kupitia minada ya hadhara ili kuondoa nafasi zozote za kuuzwa kwa bei isiyo ya ushindani kati ya kampuni ndugu.