RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16 iliyowasilishwa bungeni mjini hapa Alhamisi, imebaini udhaifu katika mradi wa bomba la usafirishaji gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es salaam.
CAG, Prof. Mussa Assad, katika ripoti yake alisema matumizi ya bomba hilo yapo chini ya kiwango na wateja wa gesi asilia hulipa bei inayofanana ilihali wapo umbali tofauti.
Mengine ni kutokulipwa kwa ankara za mauzo ya gesi asilia kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) kwenda Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kuwapo kwa kipengele cha mkataba wa mkopo kisichoridhisha na tofauti ya bei ya gesi kwa wauzaji wa gesi kwa Tanesco.
Pia, CAG amegundua mapungufu ya mifumo ya usalama katika kituo cha kinyerezi, mikataba ya uuzaji wa gesi yenye kipengele cha serikali kulipia gesi hata kama haijatumia gesi hiyo na mgogoro usio na ufumbuzi wa bei ya mabaki yaliyotokana na uzalishaji wa gesi.
Katika ripoti hiyo, CAG alisema bomba hilo lilijengwa na kampuni ya maendeleo ya petroli na Teknolojia China (CPTDC) kwa gharama ya dola za kimarekani bilioni 1.283 ambapo kati ya hizo, dola za Kimarekani bilioni 1.225 zilipatikana kama mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya Exim ya China.
Alibainisha marejesho ya fedha za mkopo huo yalitegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara.
Prof. Assad alisema katika mapitio ya mkataba wa mikopo, hata hivyo, amebaini bomba hilo lilijengwa kabla ya kutafuta wateja.
Alisema mapungufu hayo yanaathiri malipo ya mkopo kwa vile mauzo halisi ya gesi asilia yatakuwa chini ya kiwango cha makadirio ya awali cha futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku.
Pamoja na hayo, CAG alisema kwasasa Tanesco ndiyo mteja pekee wa gesi ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku ambapo makubaliano yalikuwa ni kutumia futi za ujazo milioni 80 kwa siku.
“Nashauri jitihada zaidi ziongezwe katika kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa serikali,” alisema Prof. Assad.
CHINI ASILIMIA 94
Aidha, Prof. Assad alisema matumizi ya bomba hilo yapo chini ya kiwango kwa asilimia 94 kwa sababu lilijengwa ili kuwezesha usafirishaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kupikia majumbani na kwenye magari.
Katika mapitio ya CAG, aligundua ingawa gesi ilikusudiwa kuwa na matumizi mengi, Tanesco ndiyo mteja pekee aliyeunganishwa kwenye bomba hilo na anatumia asilimia sita.
“Kiasi hicho ni pungufu futi za ujazo milioni 737.39 kwa siku ili kujaza bomba," anasema CAG katika ripoti. "Hii ni tofauti na mkataba wa mauziano na Tanesco inatumia gesi kwenye mitambo sita ya uzalishaji umeme.”
Alishauri TPDC iwasiliane na Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini ili wajadiliane ni namna gani mitambo ya uzalishaji umeme ya Tanesco itaweza kumalizika kwa wakati ili bomba la gesi litumike kwa ufanisi na kuweza kulipa mkopo wa bomba hilo kutoka benki ya Exim ya China kwa wakati.
CAG pia alitaka nguvu zaidi zielekezwe kutafuta wateja zaidi wa gesi asilia ili kuongeza mapato ya gesi na kuiwezesha TPDC kutimiza wajibu wa kulipa madeni inapostahili.
Aidha, CAG alisema kutoza bei ya gesi inayolingana kwa wateja wa gesi asilia waliopo Dar es salaam na waliopo jirani na chanzo cha gesi sio njia sahihi ya kuhamasisha upatikanaji zaidi wa wateja.
Prof. Assad alishauri TPDC kuandaa rasimu ya bei ya gesi itakayotofautisha bei za gesi zitakazokuwa zikilipwa na wateja mbalimbali kulingana na umbali kutoka chanzo cha gesi.
CAG alibainisha Tanesco haijailipa TPDC kiasi cha dola za Kimarekani milioni 61.35 za ankra ya mauzo ya gesi asilia.
Alisema TPDC na Tanesco walikubaliana serikali iweke dhamana benki kiasi kinachoweza kulipa mauzo ya gesi kwa miezi mitatu au zaidi kwa ajili ya TPDC na dhamana hiyo iwepo hadi pale Tanesco itakapolipa madeni yanayohusu mauziano ya gesi hiyo.
“Serikali haijaweza kuweka dhamana hiyo, (na) hadi Desemba 2016 jumla ya deni la mauzo kiasi cha dola za kimarekani milioni 61.35 sawa na Sh. bilioni 133.4 kilikuwa kimelimbikizwa bila kulipwa na Tanesco,” alisema.
Alisema hali ya kuchelewa kuilipa TPDC inasababisha TPDC kuchelewa kuyalipa makampuni yanayouza gesi na hivyo kuongeza hali ya sintofahamu kwenye ulipaji wa mkopo wa benki ya Exim ya China.
Kadhalika, alisema kuchelewa huko kwa malipo kunaweza kusababisha gharama zaidi za riba ambayo itatakiwa kulipwa na TPDC kwa wadai wake na kushauri TPDC iandae mpango wa kufanya malipo kwa wauzaji wa gesi na mkopo kutoka benki hiyo ili kuepuka riba kubwa.